January 27, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi watakiwa kupanda miti kuimarisha uoto wa asili

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

WANANCHI katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya wametakiwa kupanda miti ili kudumisha uoto wa asili uliopo, kupata mvua za kutosha,Matunda kwa ajili ya kuimarisha lishe ya jamii,mbao kwa uchumi imara wa wananchi

Kauli hiyo imetolewa Januari 24,2025 na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe,Jaffar Haniu wakati aliposhiriki Kampeni ya upandaji miti zoezi ambalo limefanyika katika eneo la Shule ya msingi umoja iliyopo kata ya Kyimo tarafa ya Ukukwe.

“Kila mkazi apande miti katika maeneo yake lengo letu kupata uoto wa asili pamoja na kuongeza uchumi  miongoni mwa wananchi wote “amesema Mkuu huyo wa Wilaya.

Aidha  Haniu amesema katika kutimiza hilo wilaya ya Rungwe inatarajia kupanda miche 162,000 kwa kutumia Mapato yake ya ndani ambapo wakazi wa wilaya ya Rungwe watanufaika kwa kugawiwa bure.

Haniu amesema kuwa kila mwananchi atapata miche hiyo bure ili kuhakikisha kila mkazi wa wilaya hiyo anapanda miche hiyo .

Kwa upande Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Rungwe,Renatus Mchau amesema kuwa Halmashauri ya Rungwe  kwa Mwaka huu wa fedha 2024/25 inatarajia kupanda jumla ya miti Million1.5 malengo yanayotarajiwa kutumia kwa kushirikiana na wadau wa misitu kama Wakala wa Misitu TFS -Kiwira, Mahenge Group, WAO Group na wengine wengi

Mchau  amesema kuwa jitihada hizo za upandaji miti zitafanywa kwa kushirikiana na wadau lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa maeneo yote ya Wilaya ya Rungwe yamekuwa na miti ya kutosha.

Kwa upande wake Afisa  Misitu Halmashauri  Rungwe ,Castory Makeula amesema miti iliyopo katika kitalu cha Bomani ambayo wananchi watapewa bure pamoja na taasisi mbalimbali kuwa ni pamoja na ya Matunda, Vivuli, Mbao na  kutunza vyanzo vya maji.