Na Suleiman Abeid,
Timesmajira Online, Shinyanga.
WATANZANIA wameshauriwa kujiwekea utaratibu wa kutembelea maeneo ya Hifadhi za Taifa zilizopo nchini hapana ili kufanya utalii wa ndani na kujionea vivutio mbalimbali vilivyomo katika hifadhi hizo.
Mbali ya kujionea vivutio vya wanyama na mandhari za hifadhi lakini pia fedha kidogo watakazolipa zitawezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo nchini hapana ikiwemo upatikanaji wa dawa katika zahanati,vituo vya afya,hospitali na miundombinu imara ya barabara.
Ushauri huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo wilaya ya Chato mkoani Geita, Alord Mwasalukwa ambapo amesema watanzania wanapaswa kujiwekea utaratibu wa kutembelea maeneo ya hifadhi yaliyopo nchini hapana badala ya kuwaachia wageni kutoka nchi za nje pekee yao.
Mwasalukwa amesema iwapo idadi ya watanzania wanaotembelea maeneo ya Hifadhi za Taifa zilizopo nchini hapana ni wazi pato la Taifa pia litaongezeka kutokana na fedha watakazolipa kuchangia huduma mbalimbali watakazopatiwa muda wote wanapokuwa ndani ya hifadhini.
Pia amesema Hifadhi ya Taifa ya Rubondo imetangazwa rasmi ndani ya Gazeti la Serikali mnamo mwaka 1977 na ipo katika Mkoa wa Geita wilayani Chato ambapo hifadhi hiyo pamoja na kuhifadhi mazingira lakini pia shughuli za utalii zinafanyika vyema kutokana na uwepo wa wanyama wengi ambao ni vivutio vizuri.
Baadhi ya wanyama waliomo ndani ya hifadhi hii ni pamoja na tembo,twiga, viboko,mamba,sitatunga (jamii ya swala), sokwe,nguruwe pori, ndege wa aina mbalimbali ambapo kuna waliopandikizwa na wengine ni wa asili katika kisiwa hicho.
Mwasalukwa amefafanua kuwa filamu iliyorekodiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Royal Tours imetoa mchango mkubwa kwenye hifadhi hiyo baada ya kuongezeka kwa idadi kubwa ya watalii hasa wale wa ndani na wanatarajia kuongeza idadi ya watalii kutoka idadi ya sasa hadi kufikia kupokea watalii milioni nane.
“Mara baada ya kuzinduliwa kwa filamu hiyo watu wengi wamepata muamko na kuanza kutembelea hifadhi zetu ni pamoja na watalii wanaotoka nchi za nje ambao baadhi yao kutoka kabla ya filamu hiyo walikuwa hawaijui vizuri nchi yetu ya Tanzania, lakini sasa wengi wanakuja kujionea uhalisia wa hifadhi zetu,” ameeleza Mwasalukwa.
Ameendelea kufafanua kuwa mbali ya shughuli za utalii lakini pia hifadhi hiyo ya Rubondo imekuwa ikishirikiana na jamii inayowazunguka kwa kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo ujenzi wa shule na Zahanati kama inavyoelekezwa na Serikali kuhusu suala zima la utoaji wa fedha za CSR.
“Miongoni mwa mchango wetu kwa jamii, ni ujenzi wa Zahanati katika kijiji cha Katembe wilayani Muleba mkoani Geita, ambayo pia tumeweka vifaa tiba na samani za ofisi kwa ajili ya kuwasaidia wakazi wa kijiji hicho ambao awali walikuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya,” ameeleza Mwasalukwa.
Kaimu wa huduma za utalii katika hifadhi ya Kisiwa cha Rubondo, Robert Mushi amesema mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Katembe umegharimu kiasi cha shilingi milioni 19 ambao umegawanyika katika maeneo matatu ambayo ni jengo lenyewe, pili samani za ndani na vifaa tiba vyote vikiwa vimefadhiliwa na hifadhi ya Rubondo.
Diwani wa kata ya Nyakabango, Pastory Gwanchele ameishukuru hifadhi ya Kisiwa cha Rubondo kwa kuwajengea Zahanati hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa imewaondolea kero wakaazi wa kijiji cha Katembe ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika kata nyingine.
Baadhi ya wakaazi wa kijiji cha Katembe pia wameishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka utaratibu mzuri wa wawekezaji mbalimbali kutoa kiasi cha fedha kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya kijamii (CSR) katika vijiji vinavyozunguka maeneo waliyowekeza.
Mathias Faustine ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Kijiji cha Katembe amesema wamefarijika kutokana na kujengewa Zahanati hiyo ambayo imemaliza changamoto ya baadhi ya akinamama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kufariki njiani wakiwa wanafuata huduma za afya katika kata jirani.
“Tunawashukuru wenzetu wa Hifadhi ya Rubondo kwa ujenzi wa Zahanati hii, kwa kweli wamenusuru maisha ya akinamama zetu wajawazito ambao mara nyingi walifia njiani wakati wakipelekwa kwenda kujifungua kwenye vituo vya afya katika kata jirani, na tunaishukuru Serikali yetu kwa kuweka utaratibu huu mzuri,” ameeleza Faustine.
More Stories
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25