July 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi wakaribishwa TPHPA kujifunza teknolojia ya mimea


Na Joyce Kasiki, Dar

MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imewataka wakulima, wafanyabiashara wa mazao na wananchi kutembelea banda lake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba ili kujifunza teknolojia za kisasa za kudhibiti visumbufu vya mazao, kupata elimu kuhusu matumizi salama ya viuatilifu na taratibu za kuuza mazao katika masoko ya Kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika maonesho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Joseph Ndunguru, alisema ushiriki wa mamlaka hiyo unalenga kuwakutanisha wadau na huduma mbalimbali zinazotolewa ili kuongeza tija ya uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza fursa za masoko kwa wakulima.

Alisema TPHPA inasimamia afya ya mimea na matumizi sahihi ya viuatilifu, huku ikitoa teknolojia za kisasa za kudhibiti visumbufu vya mazao, hatua inayochangia kuongezeka kwa uzalishaji, ajira na ushindani wa mazao ya Tanzania katika soko la ndani na nje ya nchi.

Profesa Ndunguru alisema Mamlaka hiyo pia ina jukumu la kuhakikisha mazao yanayouzwa nje yanakidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa katika masoko ya kimataifa.

Alibainisha kuwa hivi karibuni Tanzania imefanikiwa kufungua soko la ndizi mbichi nchini Afrika Kusini, pamoja na soko la mazao 10 nchini China, yakiwemo tangawizi, vitunguu, kitunguu saumu na kabichi.

Alisema wafanyabiashara wanaotaka kuuza mazao nje ya nchi wanaweza kupata mwongozo wa taratibu zote muhimu katika banda la TPHPA, ikiwemo masharti ya masoko mbalimbali na namna ya kuzingatia viwango vinavyokubalika Kimataifa.

Aidha, alisema banda hilo linaonesha teknolojia za udhibiti wa visumbufu kwa njia za kibaolojia, ikiwemo matumizi ya wadudu rafiki na usajili wa viuatilifu hai kupitia Kituo cha Taifa cha Udhibiti wa Visumbufu kwa Njia za Kibaolojia kilichopo Kibaha.

Aliongeza kuwa wananchi pia watapata fursa ya kujifunza kazi zinazofanywa na Benki ya Taifa ya Mbegu iliyopo Arusha, ikiwemo uhifadhi wa mbegu za asili, upatikanaji wa baadhi ya mbegu hizo pamoja na mchango wake katika utafiti wa mbegu zinazostahimili ukame na magonjwa.

Profesa Ndunguru aliwataka wakulima, wafanyabiashara wa mazao na wadau wengine wa sekta ya kilimo kutumia fursa ya Maonesho ya Sabasaba kutembelea banda la TPHPA ili kupata elimu, teknolojia na huduma zitakazowawezesha kuongeza tija katika uzalishaji na kufikia masoko yenye ushindani ndani na nje ya Tanzania.