November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi waipongeza TBA kwa ubora wa miradi

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Mbeya

BAADHI ya wananchi waliotembelea Banda la Wakala wa Majengo nchini (TBA) wameupongeza Wakala huo kwa ubora wa majengo katika miradi yao wanaoitekeleza.

Wakizungumza katika Banda hilo wananchi hao wamesema,TBA wamekuwa wakitekeleza miradi yao kwa ubora lakini wamekuwa wakijenga majengo mazuri.

Aneth Mushi kutoka chuo Kikuu Mzumbe Tawi la Mbeya amesema,moja ya banda ambalo amevutiwa nalo ni pamoja na banda la TBA kutokana na kazi wanayoifanya katika miradi mbaimbali hapa nchini ikiwemo mradi wa ujenzi wa Mahakama .

“Nimevutiwa na ujenzi wa majengo mbalimbali,nawasishi wananchi wafike katika banda hilo kujionea majengo na miundombinu mizuri inayongwa na Wakala huo ,mimi binafsi nimevutiwa baada ya kuona ujenzi wa mahakama za Mwanzo ambazo nafanya mazoezi ,ni majengo mazuri ya kuvutia.”amesema

Naye Amina Athumani mwanafunzi wa Ruaha Catholic University Iringa amesema TBA wanafanya ubunifu wa majengo mazuri ambayo alikuwa hajui kama TBA ndiye amebuni na kujenga majengo hayo.

Akizungumza katika Banda hilo Mhandisi Haruna Kalunga kutoka TBA ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wananchi kutembelea banda lao ili kujionea wao wenyewe shughuli hasa majengo wanayoyajenga lakini pia kujionea miradi inayogusa moja kwa moja kwenye kilimo.

Amesema moja ya miradi hiyo ni mradi wa teknolojia mpya ya vihenge vya kisasa ambavyo vinachukua eneo dogo kwenye kutunza nafaka kwa ajili ya usalama wa chakula.

“Teknolojia hii inafanya utunzaji wa mahindi bila kutumia dawa ,sisi kama TBA tulihusika kwenye mradi huu kuanzia hatua ya awali mpaka ukamilishaji wa huo ambao Mshitiri alikuwa ni Wakala wa Chakula TFRA .”amesema Mhandisi Kalunga

Amesema,mradi umetekelezwa kwenye mikoa Nane ambapo kwa upande wa Nyanda za Kusini umetekelezwa maeneo ya Sumbawanga (Mkoa wa Rukwa ),mkoa wa Songwe,Makambako (mkoa wa Njombe),na Songea (mkoa wa Ruvuma).

“Kwa hiyo mradi huu ni mzuri tumeutekeleza kwa asilimia mia moja tumeshakabidhi kwa Mshitiri na hivi tunavyozungumza tayari Mshitiri ameshanunua mahindi na ameshahifadhi kwenye maghala.

 Kwa upande wake Hassan Mbano kutoka kitengo cha Miliki amesema,wakala huo pia umekuwa ukifanya miradi ya ujenzi wa nyumba za kupangisha watumishi wa umma na wananchi wa kawaida lakini pia kukopesha nyumba kwa watumishi na ujenzi wa nyumba za viongozi na ofisi.

“Tunatekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba mbalimbali za viongozi ,nyumba za watumishi kwa ajili ya kupangisha na kuuza na zipo katika mikoa tofauti hasa mkoa wa Dar es Salaam na Dodoma,kwa mkoa wa Mbeya tumefanya mradi wa ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya.”amesema na kuongeza kuwa

“Kwa hiyo zipo kazi nyingi tunafanya ikiwa ni pamoja na kukopesha nyumba kwa ajili ya watumishi ambao wanalipia kidogo kidogo hadi anapofikia hatua ya kustaafu anakuwa amemaliza deni lake na kumiliki nyumba badala ya kusubiri kujenga kwa kutumia mafao ya pensheni.”