Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
KAMISHNA wa Ardhi ,Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Nathaniel Nhonge amewataka wananchi kulipa kodi ya ardhi mapema badala ya kusubiri mpaka waepelekwe mahakamani kwa kukaidi kulipa kodi hiyo.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu suala la ulipaji kodi ya ardhi huku akisema kila anayemiliki ardhi anapaswa kulipa kodi hiyo kwa mujibu wa sharia.
“Kipindi hiki tunapoelekea mwisho wa mwaka ndio wananchi wengi wanapenda kulipa kodi,kwa hiyo tunawaasa wananchi wafanye hivyo kwa siku hizi zilizobaki kabla mwaka huu haujaisha ili wasiingie Januari 2022 wakiwa hawajalipa kodi kwani wataanza kulipa na riba.”amesema Nhonge
Amesema,Kodi ya ardhi ni wajibu kwa anayemiliki ardhi kuilipa kwa mujibu wa sheria kwa kodi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na Taifa kwa ujumla.
“Kodi hii inalipwa kwa mwaka ,kwa hiyo kila mwaka mwananchi unawajibika kulipa kodi ya pango la ardhi,kwa maana hiyo mwaka ninaouzungumza hapa ni kuanzia Julai Mosi hadi Juni 30 ya mwaka unaofuata…, hicho ndio kipindi cha kulipa kodi kwa mwaka,
“Lakini pia kwenye sheria imeweka utaratibu kwamba katika kipindi cha miezi sita yaani kuanzia Julai Mosi Mpaka Desemba 31 ndicho kipindi mtu analipa kodi bila kutozwa riba,kwa maana kwamba ikifika Januari Mosi mwaka unaofuata unaanza kutozwa na riba ya asilimia moja ya kodi unayolipa , kwa maana kwamba umechelewa japo upo ndani ya mwaka mmoja wa kulipa, sasa sisi msisitizo wetu ni kuwataka na kuwaomba wananchi walipe kodi ya ardhi katika kipindi hiki cha miezi sita kabla ya kuanza kuongezeka riba ya asilimia moja kwa kila mwezi.”
Aidha amesema kwa wale ambao wana madeni makubwa upo utaratibu wa lulipamkidogo kidogo ili kumpunguzia mwananchi maumivu hadi mteja anapomaliza deni lake huku akisema wanapoona kwamba bado kodi hiyo hailipwi watumishi wa sekta ya ardhi wamekuwa wakisambaza hati za madai kwa wahusika.
“Sheria imeelekeza kwamba unapoona kodi haijalipwa ndani ya muda basi unapeleka hati ya madai kwa mwananchi huo ili kutumia utaratibu wa kisheria wa kuusanya kodi hiyo ,hivyo tunampa hati ya siku 14 kama huo utakwisha kodi haijakusanywa basi tunawapeleka kwenye mahakama zetu ambazo ni mabaraza ya ardhi na Nyumba ya wilaya ambako huko nia thabiti ya wizara ni kukusanya kodi ya pango la ardhi.”amesema Nhonge
Nhonge amesema,ili kurahisisha suala hilo ,wameweka utaratibu wa kulipa kupitia namba ya simu lakini pia kutumia wavuti ya wizara hiyo lakini pia kwa kufika katika ofisi za mikoa,wilaya hadi Makao Makuu lakini pia wameanzisha kituo cha mawasiliano kwa wateja kurahisisha huduma kwa wananchi kuhusu masuala ya ardhi.
“Nia ya wizara ni kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kwa wananchi juu ya ulipaji wa kodi ya pango la ardhi kwa sababu tunaamini kwamba kila penye haki pana wajibukwa hiyo mwananchi ana haki ya kumiliki ardhi lakini pia anao wajibu wa kuhakikisha analipa kodi ya pango la ardhi.”alisisitiza
Akizungumzia kuhusu makusanyo ya kodi hiyo amesema,kwa mwaka huu wa fedha wizara hiyo imepanga kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 221 .
Hata hivyo amesema,Serikali ipo kwenye mkakati wa miaka kumi wa kupanga na kupima ardhi ili wananchi wengi zaidi wamiliki ardhi kwa kuwashirikisha makampuni ya kupanga na kupima ili kuongeza kasi ya upimaji ardhi nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Denis Masami alisema,mpaka sasa tayari wamekusanya zaidi ya shilingi bilioi 60 huku akisema,katika kipindi hiki watakusanya zaidi kwani ndio kipindi cha wananchi kulipa kodi.
“Hiki ndio kipindi ambacho ambacho watu wengi wanapenda kulipa kodi kwani ndio mwishoni mwa mwaka,lakini pia kindi cha Juni na ni kipindi cha Juni watu hulipa sana kodi kwani ndio mwisho wa mwaka wa fedha.”amesema Masami
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi