*Waendesha bodaboda watakiwa kuwa mabalozi wa amani
*Polisi wasisitiza utii wa sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali,kulinda maisha
Na Judith Ferdinand,Timesmajira Online-Mwanza
Wito umetolewa kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza kuepuka kujihusisha na vurugu kama zilizotokea Oktoba 29,2025 huku waendesha bodaboda wakitakiwa kuwa mabalozi wa amani.
Hayo yameelezwa Novemba 29,2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP. Wilbrod Mutafungwa,wakati akizungumza na maofisa usafirishaji( bodaboda) wa Kanda ya Igoma wilayani Nyamagana mkoani hapa.

Ikiwa ni muendelezo wa jeshi la polisi Mkoa wa Mwanza kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya kijamii ili kuimarisha usalama na kudhibiti uhalifu.
DCP.Mutafungwa,amesisitiza kuwa matatizo yoyote ya kisheria yashughulikiwe kwa kufuata taratibu badala ya kujichukulia sheria mkononi huku akuwasihi waendesha bodaboda kuwa mabalozi wa amani na usalama kwa kutoshiriki au kushawishiwa kushiriki vitendo vya uchochezi au uharibifu wa mali.
“Kupitia elimu na ushirikiano, tumeweza kuzuia uhalifu mkubwa uliokuwepo awali.Hatuna nchi nyingine ya kwenda kuishi, tukiharibu hii, tunajiangamiza wenyewe,”amesisitiza DCP.Mutafungwa.
Sanjari na hayo DCP. Mutafungwa, amesema ongezeko la ajali za barabarani linatokana na uzembe wa baadhi ya waendesha vyombo vya moto hivyo akataka kila mmoja kuwajibika ipasavyo kukomesha ajali hizo.
Pia amesisitiza utii wa sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani ni wajibu wa kila mtumiaji wa barabara huku akiwaonya dhidi ya makosa hatarishi kama vile kuendesha bila kofia ngumu, kupuuza taa za barabarani, kubeba abiria zaidi ya mmoja, kuendesha bila leseni au mafunzo rasmi ya udereva.
“Makosa haya yamekuwa chanzo cha vifo na ulemavu kwa watumiaji wa barabara,” amesema DCP. Mutafungwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, SSP. Ibrahim Sunday, amewataka maofisa usafirishaji kuhakikisha wanakuwa na bima halali, leseni ya udereva na kufuata sheria zote za usalama barabarani.
“Dereva asiye na sifa ni tishio kwa maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara,” amesema SSP.Sunday.

Naye, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana,SSP.Virginia Sodoka, amewataka waendeleze mshikamano na kushirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu au vitendo vyovyote vinavyohatarisha usalama kwenye sekta ya usafirishaji ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Akizungumza kwa niaba ya maofisa usafirishaji wa Kanda ya Igoma, Katibu wa Umoja wa Waendesha Pikipiki Mkoa wa Mwanza, Kudra Salum, ameahidi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za kihalifu na kuchukua hatua dhidi ya wanachama wanaokiuka sheria na kujihusisha na vitendo vya uhalifu.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi