Na Fresha Kinasa, TimesMajira Online, Mara
WANANCHI wa Kijiji cha Kataryo Kata ya Tegeruka Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Mkoa wa Mara wameamua kujenga zahanati yao kwa kutumia nguvukazi na michango ya fedha zao, pamoja na baadhi ya wadau wa maendeleo wa kijiji hicho.
Kijiji cha Kataryo ni moja ya vijiji vitatu vya Kata ya Tegeruka na vingine ni Mayani na Tegeruka huku Kata hiyo ina zahanati moja inayohudumia vijiji vyote na imejengwa kijijini Mayani.
Kutokana na hatua hiyo Diwani wa Kata hiyo, Alpha Modikae Mashauri amechangia saruji mifuko 50 huku akiahidi kuendelea kuchangia ujenzi huo.
Pia Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijni Prof. Sospeter Muhongo akianza kwa kutoa michango yake,saruji mifuko 200, akiahidi kuendelea kuwaunga mkono wananchi hao.
Hayo yamesemwa Juni 3, 2024 kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo ambapo pia imefafanua kuwa Wananchi jimboni humo wanaendelea na ujenzi wa zahanati za vijiji vyao kwa kushirikiana na Madiwani wao huku Mbunge wa Jimbo ili kuhakikisha kila Kijiji kinakuwa na zanahati.
Jimbo la Musoma Vijijini lina Kata 21 zenye vijiji 68 na vitongoji 374 na kila kijiji kimedhamiria kujenga zahanati yake.
Ambapo kwa sasa Jimbo zima lina zahanati 29 zinazotoa huduma za afya kati ya hizo 25 ni za serikali na 4 ni za binafsi huku vituo vya afya vikiwa 6 na Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ikiwa ni moja.
Taarifa hiyo imesema zahanati mpya 16 zinaendelea kujengwa katika vijiji vya Burungu, Butata, Chanyauru, Chimati, Chirorwe, Kaburabura, Kakisheri, Kataryo, Kurukerege, Kurwaki, Kwikerege, Maneke, Mabuimerafuru, Nyabaengere, Nyambono na Nyasaungu.
Ambapo utaratibu unaotumika ni Wanakijiji wanabuni mradi na kutayarisha eneo la ujenzi kisha wanapewa ushauri kutoka kwa Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
“Serikali hukamilisha ujenzi wa zahanati na kuweka vifaa tiba na wafanyakazi wanaohitajika,wadau watusaidie kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo kabla ya Disemba 2024.imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa upande wake Rhoda Samson Mkazi wa Kataryo amesema kuwa iwapo kila Kijiji kikiwa na zahanati itasaidia kuimarisha huduma za afya na Wananchi kupata huduma hizo karibu na makazi yao.
More Stories
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika
TANESCO yarudisha shukrani kwa jamii