Na Lubango Mleka, TimesMajira Online Musoma Vijijini.
WANANCHI wa Kijiji cha Wanyere Kata ya Suguti Halmashauri ya Musoma Mkoani Mara, wameamua kujenga shule ya sekondari ili kutatua changamoto ya wanafunzi kutembea umbali wa kilomita 18.Umbali huo sawa na kilomita 32 kwenda shule na kurudi nyumbani kwa siku pamoja na kutatua kero ya mrundikano wa wanafunzi darasani.
Hayo yalibainishwa na baadhi ya wanakijiji waliojitokeza kufanya usafi katika eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo kutoka vitongoji sita vya kijiji hicho waliojitambulisha kwa majina ya Judith Daudi, Elias Ndala na Olipa Jactan.
“Tumeamua kujenga shule ya sekondari hapa kijijini kwetu Wanyere ili kutatua changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu wa kilometa 18 kufuata masomo,pia kuondoa mrundikano darasani kwenye shule yetu ya kata, tunawaomba wadau na Mbunge wetu Sospter Muhongo atuunge mkono ili tuweze kutimiza lengo letu la kuwa na shule ya sekondari hapa kijijini kwetu,” amesema Judith.
Eliasi Ndala ameeleza kuwa wameamua kuunga mkono juhudi za Rais Samia Hassan Suluhu katika sekta ya elimu kwa kutimiza ndoto ya watoto wao kupata elimu ya sekondari hadi chuo kwa kuanza na ujenzi wa shule kijijini kwao Wanyere.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho Thomas Chibunu, amesema kuwa anatambua kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia ni sikivu sana hivyo itawaunga mkono, huku akiwaomba wadau wote wa maendeleo nchini, wananchi na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini kuwaunga mkono kwa hali na mali kwa kuchangia kupitia akaunti ya serikali ya kijiji .
Kaimu Mtendaji wa kijiji hicho Hanifa Ibrahim amesema kuwa wanamshukuru Mungu, mpaka sasa wanaendelea vizuri tangu wameanza ujenzi huo muitikio wa wananchi umekuwa mkubwa kadri siku hadi siku zinavyozidi kuongezeka kwa kujitolea kusafisha eneo, kusomba mchanga na mawe, kuchimba msingi na kung’oa visiki,matumaini yake jambo hilo litafanikiwa.
Katika kuunga juhudi hizo za wananchi, Mbunge wa Jimbo hilo Sospter Muhongo ameanza kwa kuchangia ujenzi huo kwa kutoa Saruji mifuko100.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato