Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto
Wananchi wa vijiji vitano katika Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga watanufaika na mradi wa maji Irente- Yoghoi- Ngulwi- Bombo unaojengwa kwa gharama ya zaidi ya milioni 578 (578,175,639) ambao ukifikia asilimia 90.
Mradi huo utanufaisha wananchi 6,239 wa vijiji vya Ngulwi, Bombo, Chumbageni, Handei na Miegeo.
Hayo yamesemwa Juni 14, 2023 na Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Abdallah Shaib Kaim alipofika kufungua mradi huo uliopo Kata ya Ngulwi.
Sizinga amesema mradi huo unaendelea kutekelezwa na RUWASA chini ya Mkandarasi Buzubona & Company Ltd kwa mkataba uliosainiwa Mei 20, 2022, na unategemea kukamilika Juni 30, 2023.
Amesema kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa chanzo kipya cha maji,ukarabati wa matanki mawili ambao ujenzi wake ni asilimia 100,uchimbaji wa mitaro na kufukia mita 13,500 asilimia 95, ulazaji wa bomba mita 13,500 asilimia 90.
“Uunganishaji wa bomba na fitting zake asilimia 70, ujenzi wa vituo 18 (vilula) vya kuchotea maji asilimia 90, na ujenzi wa break pressure tank (BPT) mbili na uwekaji wa uzio katika matanki matatu ya maji vimekamilka kwa asilimia 100,”amesema Sizinga.
Sizinga amesema kazi ambazo hazijakamilka ni ulazaji wa bomba mita 2,800 pamoja na kuunganisha maji katika vituo vinane (8) vilivyobakia.
Sizinga amesema RUWASA wanampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassa kwa jitihada zake za kuhakikisha Watanzania wanapatiwa maji mijini na vijijini, kwani ameendelea kupeleka fedha za miradi ya maendeleo, huku akiahidi kuwa fedha hizo watazisimamia vizuri ili ziweze kuleta tija na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shabaan Shekilindi amempongeza Rais Dkt. Samia kwa kuweza kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo, kwani utawakomboa wananchi hivyo kuondokana na shida ya maji pamoja na kuendelea kuboresha sekta ya maji hususani Mji wa Lushoto.
Kwani ameweza kutoa kiasi cha bilioni moja ili kufanyia ukarabati mkubwa miundombinu ya maji kwenye mji huo.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo akizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya mradi wa maji Irente kufunguliwa, amesema yeye na wasaidizi wake kwenye mkoa huo wamejipanga kutekeleza miradi ya maji kwa ubora wa hali ya juu ili kukidhi matarajio ya Rais Dkt. Samia ya kuhakikisha maji yanapatikana mijini na vijijini.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba