March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi wa Nzega waahidiwa neema

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online-Nzega

MGOMBEA Mwenza wa kiti cha Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali chini ya chama hicho imeweka mikakati ya kuanzisha kituo cha kisasa cha utafiti wa mbegu nchini kitakachojengwa wilayani Nzega.

Dkt. Nchimbi amesema hayo,Oktoba 4, 2025 kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Utwale,kijiji cha Itobo, Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.

Amesema, dhamira ya kuanzishwa kwa kituo hicho ni kuendelea kuboresha sekta ya kilimo nchini pamoja na kukuza uchumi kwa wakulima.

Akiwa katika Jimbo la Bukene,Dkt. Nchimbi amesema, tayari Serikali imenunua vifaa vya kupima ardhi katika wilaya zote nchini, huku akieleza kuwa, hatua hiyo imesaidia kupandisha thamani mazao na kilimo kuongezeka kwa asilimia tano kila mwaka.

Pia amesema, kwenye mifugo Serikali imepandisha bajeti kutoka bilioni 66 hadi bilioni 400, ikiwa pamoja na kuongeza ujenzi wa majosho na dawa za mifugo ambavyo vimenufaisha wafugaji wengi.

Hata hivyo amesema, miongoni mwa miradi ya maendeleo itakayopelekwa kwenye Jimbo la Bukene ni pamoja na ujenzi wa skimu za umwagiliaji tisa, ujenzi wa soko la kisasa na ujenzi wa kituo cha kupooza umeme kitakachojengwa Nzega.

Aidha akihutubia wananchi wa Jimbo la Nzega vijijini, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa stendi ya mabasi uliopo katika Wilaya ya Nzega mkoani Tabora,ametaja miradi ya maendeleo watakayo nufaika nayo wakazi wa eneo hilo kuwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya afya viwili na zahanati 10, shule za msingi nne na sekondari sita.