January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi wa Kwemasimba, Korogwe wapata maji ya bomba

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online Korogwe

WANANCHI wa Kijiji cha Kwemasimba, Kata ya Vugiri, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wameondokana na adha ya kutafuta maji umbali mrefu baada ya Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuwajengea mradi wa maji.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim akifungua koki ya maji kama ishara ya kufungua mradi wa maji Kwemasimba uliopo Kijiji cha Kwemasimba, Kata ya Vugiri, Tarafa ya Bungu, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga huku wa pili kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini Timotheo Mnzava.

Akisoma taarifa ya mradi wa maji Kwemasimba Juni 15, 2023 kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa, amesema mradi huo utanufaisha wananchi 2,731 wa kijiji cha Kwemasimba.

Mhandisi Tupa amesema Desemba 29, 2021, RUWASA iliingia mkataba na Kampuni ya M/s Build All Contractors Ltd ya Dar-es-Salaam kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji Kwemasimba, lengo likiwa ni kutoa huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kwa wananchi 2,731.

“Gharama za ujenzi wa mradi huu zaidi ya milioni 481(481,215,973) kupitia Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF), na mkandarasi ameshalipwa hati ya malipo namba moja yenye jumla ya zaidi ya milioni 130(130,720,812).

Aidha wananchi wa Kijiji cha Kwemasimba wamechangia mradi huu kwa kutoa maeneo yao ili kuwezesha kujengwa kwa miundombinu ya maji.

Tupa amesema kazi zilizotekelezwa kwa mujibu wa mkataba ni ujenzi wa banio (intake) umekamilika kwa asilimia 100, ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 75,000 umekamilika kwa asilimia 98 pamoja na ujenzi wa bomba lenye urefu wa mita 5,706 umekamilika kwa asilimia 100.

“Ujenzi wa BPT tatu umekamilika kwa asilimia 98, vituo vya DP’s (vilula) 10 umekamilika kwa asilimia 100, ujenzi wa ofisi ya CBWSO (watumia maji) umefikia asilimia 30, na kwa ujumla mradi upo asilimia 75 ya utekelezaji, na wananchi wanapata huduma ya maji kama ilivyokusudiwa na serikali,”amesema Tupa.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Mhandisi William Tupa (kulia) akitoa maelezo huku akionesha mchoro wa mradi wa maji Kwemasimba kwa wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa.

Tupa amesema wanaishukuru serikali kwa kutatua kero ya maji kwa wananchi wa Kijiji cha Kwemasimba, ambapo Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa aliweza kufungua mradi huo na kupanda miti.

Kiongozi huyo amesema miradi hiyo inatolewa fedha nyingi ili iweze kuwasaidia wananchi kupata maji safi ya bomba karibu na makazi yao.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha nyingi za miradi mbalimbali ikiwemo ya maji, kwani itasaidia kumtua mama ndoo kichwani kwa kupata maji ya bomba karibu yake.

Wananchi wa Kijiji cha Kwemasimba hivi karibu walimuhakikishia Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo kuwa sasa hawatahama tena Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ili kwenda Halmashauri ya Mji Korogwe ili kupata huduma za kijamii ikiwemo maji, umeme na barabara.