March 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Vunjo watatua kero ya barabara,wataka zahanati yao

Na Martha Fatael, Moshi

HALI ya kiuchumi kwa wananchi wa Kijiji Cha Mero kata ya Kirua vunjo Mashariki wilaya ya Moshi, inatarajiwa kuimarika baada ya kukamilisha ukarabati wa barabara zinazowezesha wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya mkoa kufika kijijini hapo.

Barabara hiyo yenye urefi wa Km 12 inajengwa Kwa gharama ya zaidi ya Sh Mil 10 ikiwa ni mchango wa wakazi wa Kijiji hicho waishio nje ya mkoa wa Kilimanjaro (LEKIDEA).

Wakizungumza kijijini hapo,Ewald Umbella na Carima Mbishi, wamesema awali walilazimika kuuza ndizi na Parachichi, Kwa bei ya hasara kutokana na gharama kubwa ya kufikia masoko ya Uchira,Himo na nje ya mkoa.

Wamesema,sasa magari ya mizigo kutoka masoko ya mazao ndani na nje ya mkoa Kilimanjaro, yanaweza kuingia na kutoka kijijini hapo, mwaka mzima.

“Kwa ujenzi wa barabara hii kwa nguvu zetu itafungua fursa za kiuchumi na kurahisisha huduma za afya na Elimu kijiji hapa,…pia kibiashara ikiendelea kuimarika” amesema Umbella.

Wamesema bei ya mkungu wa ndizi wa wastani wa Sh 9,000 waliuza Sh 3,000,huku gunia la Parachichi wakiuza Sh 20,000 badala ya Sh 80,000, kwani wanunuzi walitumia gharama kubwa kufika kijijini humo.

Kuhusu Elimu walisema wanafunzi wa shule za msingi Iwa, Laso, Msufini, Mrumeni na shule za sekondari Kirua vunjo Mashariki na Kisomachi sasa Wana uhakika wa kwenda na kurudi shule Kila siku.

Mapema mwenyekiti wa kijiji hicho, Evod Malyawere, amesema barabara hiyo itawezesha wanawake wajawazito na watoto kuzifikia huduma za afya nje ya kijiji tofauti na hali ilivyokuwa awali.

“Sasa wananchi wanaweza kwenda zahanati ya Karumeli na kituo Cha Afya Kirua vunjo magharibi ambavyo vinapakana na Kijiji chetu” amesema.

Aidha wananchi hao wameomba serikali kuongeza msaada kwani barabara hizo zinahitaji kujengewa mifereji ili zisiharibiwe na mvua hususan kipindi hiki cha masika.

Hata hivyo wananchi hao katika hatua nyingine wameomba wadau na serikali kwa ujumla kuwasaidia ujenzi wa zahanati ya kijiji kwani tayari mwananchi mmoja amejitolea Ekari 2.5 za ardhi Kwa ajili hiyo.