Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbarali
MGOMBEA wa Jimbo la Mbarali mkoani Mbeya kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Bahati Ndingo amesema Wilaya hiyo imetengewa fedha za bajeti kwa ajili ya ukamilishaji wa uchimbaji wa mabwawa saba ya umwagiliaji yatakayosaidia wakulima kuachana na utegemezi wa mito na kuwawezesha kulima kwa uhakika mwaka mzima, hata kipindi cha ukosefu wa mvua.
Akizungumza Septemba 14, 2025, wakati wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mswiswi kata ya Kongolo wilaya hapa Ndingo.
“Mabwawa haya yatakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Mbarali. Hata kama mvua zitakuwa haba, mabwawa yatabaki kuwa nguzo muhimu kwa kilimo. Tuna safari kubwa na Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo nawaomba muwe na imani nasi na kutoa kura nyingi kwa CCM” Oktoba 29.”

Ndingo ameeleza kuwa Rais Samia amedhamiria kubadilisha kilimo cha Mbarali kuwa cha kisasa, kupitia fedha zilizotengwa na Bunge kwa ajili ya ukamilishaji wa mabwawa hayo ya umwagiliaji.
Aidha, amesema wilaya hiyo kwa sasa ina vituo vya afya 10 kati ya kata 20, na katika Ilani ya CCM 2025–2030 kipo kipengele cha kujenga vituo vingine vitano vya afya. Pia wito kwa wananchi kuichagua CCM katika nafasi zote ili kuendeleza maendeleo.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM pia ni Mgombea ubunge Jimbo la Makambako ,
Daniel Chongolo ambaye ni Mratibu wa Kampeni za CCM Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, amewataka wanachama wa chama hicho kuachana na mazoea ya kutojitokeza kupiga kura.
“Ikifika Oktoba 29, kila mmoja asitegemee mwenzake kwenda kupiga kura. Tukibaki na mazoea hayo, matokeo yake kura zinapungua. Tunapaswa kubadilika, maana tunaratibu mikoa minne — Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa,”amesema Chongolo.
Ameongeza kuwa akiwa Iringa ameona mikakati madhubuti ikianzia ngazi ya matawi hadi kata, ili kuhakikisha wananchi wanashawishiwa kupiga kura kwa wingi na kukipatia CCM ushindi katika ngazi zote za uongozi.
Kwa upande wake, Mbunge Mteule wa Viti Maalum mkoa wa Mbeya,Suma Fyandomo amesema Mbarali ni miongoni mwa wilaya vinara wa kilimo cha mpunga, na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia imetoa zaidi ya Sh bilioni 80 kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji, hatua iliyobadilisha maisha ya wakulima wengi.
Jeremiah Makao ni Diwani Mteule wa kata ya Rujewa amesema kuwa mgombea wa Jimbo hilo ameweza kutekeleza miradi aliyohaidi kwa wananchi akishirikiana na madiwani hivyo bado anayo nafasi ya kuchaguliwa na wananchi aweze kutekeleza miradi mingine iliyobaki.


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako