Na Mwandishi Wetu,TimesMajiraOnline, Makambako
KUKAMILIKA kwa ujenzi wa madarasa sita, vyoo pamoja na miundombinu ya maji kumewezesha Shule ya Msingi Makatani kuanza kutoa elimu kwa wanafunzi wa Kata ya Makatani waliokuwa wakikabiliwa na adha ya kutembelea umbali mrefu.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makatani, Zawadi Salehe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na jinsi miundombinu hiyo iliyojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ilivyosaidia kutatua changamoto ya wanafunzi kupata elimu mbali na wanakoishi.
Mwalimu Salehe amesema kutokana na wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda kusoma Shule ya Msingi Kiumba, Lyamkene na Ilangamoto, wazazi waliona hiyo ni kero kubwa hivyo waliibua mradi wa ujenzi wa shule.
Amesema wananchi walianza ujenzi wa shule hiyo kwa kuanza na madarasa matatu na ofisi na ujenzi wake waliufikisha hatua ya boma.
Baada ya kufikia hatua hiyo amesema walipeleka maombi TASAF ili iwasaidia kujenga shule.
Kwa mujibu wa Mwalimu Salehe, TASAF imejenga vyumba sita vya madarasa, vyoo na miundombinu ya maji ambavyo vyote vimekamilika na kuanza kutumika.
Amesema shule hiyo imeanza kufanyakazi kuanzia Januari, mwaka huu ikiwa na wanafunzi wa darasa la awali hadi la nne jumla wakiwa 167 wakiume 81 na kike 86.
Amesema watoto hao wamehamishiwa shuleni hapo kutoka shule ya msini Kiumba, Lyamkene na Ilangamoto na kwamba watoto walioanzia shuleni hapo kwa sasa ni wale wa darasa la awali.
Amesema ujenzi wa miundombinu hiyo unasaidia maendeleo ya kitaalum kwenda vizuri, kwa sababu shule ina walimu sita na kulingana na Ikama ya walimu na idadi ya wanafunzi inajitolesheza vizuri.
Kuhusu mwamko wa wazazi kupeleka watoto kusoma shuleni hapo, Salehe anasema ni mkubwa kwa sababu idadi ya wanafunzi inazidi kuongezeka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Makatani, Samson Lukogera (62), amesema waliamua kuomba TASAF iwasaidie ujenzi wa shule hiyo baada ya kuona watoto wanatembea umbali mrefu kwenda shule ya Kiumba na Lyamkena.
“Kwa hiyo tuliona wanafunzi hawana uwezo wa kutembea umbali mrefu, hivyo tuliona tuanzishe ujenzi wa shule na tunashukuru TASAF tuliwaomba watusaidie,” alisema Lukogera.
Amesema baada ya TASAF kukubali na wananchi waliunga mkono uamuzi huo kwa kuchangia asilimia 10 ya nguvu kazi ili kufanikisha ujenzi huo.
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Esther John (9) amesema anaishukuru TASAF kwa kufanikisha kuanza kwa shule hiyo kwa sababu ameondokana na adha ya utembea umbali refu kwenda kusoma Kiumba.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini