March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi kisiwani Ukara wahimizwa kutumia nishati safi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Ukerewe

Wananchi wa Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza,wamehimizwa kutumia nishati safi ya kupikia ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt .Samia Suluhu Hassan katika jitihada za utunzaji wa mazingira nchini.

Rai hiyo imetolewa na Jumuiya inayotangaza Maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita na Chama Cha Mapinduzi (CHAMATA ASSOCIATION),wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Taifa Beatrice Nyamisango,katika kata ya Bwisya kijiji cha Nyang’ombe wakati akigawa mitungi ya gesi kwa wananchi waliojitokeza kuelezea mafanikio ya Rais Samia kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.

Makamu Mwenyekiti CHAMATA Association Taifa,Beatrice Nyamisango,kushoto akimkabidhi mtungi wa gesi mmoja wa wakazi wa Kata ya Bwisya kijiji cha Nyang’ombe

Ambapo Beatrice,amewaeleza wananchi wa maeneo hayo, umuhimu wa kutunza mazingira kwa kuepuka kukata miti hovyo kwa ajili ya nishati ya kupikia na kuhamasisha nishati safi ya gesi yenye faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuokoa muda katika matumizi yake.

Kwa upande wake Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe,Shoo,ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2025/26 Serikali imetenga kiasi cha milioni 62 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa viwili na matundu sita ya vyoo katika kijiji cha Nyang’ombe.

“Mama Samia amefanya mambo mengi makubwa,sasa hivi kuna hospitali kubwa yenye hadhi ya rufaa inajengwa,kwa kweli wanaukerewe hatuna cha kufanya zaidi ya kutiki Oktoba,”amesema Sabina Malegesi mkazi wa kijiji cha Nyang’ombe.

Makamu Mwenyekiti CHAMATA Association Taifa,Beatrice Nyamisango,akiwa amemshikia kipaza sauti(mic)mmoja wa wakazi wa Kata ya Bwisya kijiji cha Nyang’ombe, kwa ajili ya kutoa maoni yake wakati Jumuiya hiyo ilipo tembelea kijijini hapo kugawa mitungi ya gesi pamoja na kuelezea mafanikio ya Dkt.Samia Suluhu Hassan

CHAMATA Association wanaendelea kuwafikia wananchi maeneo mbalimbali kwa ajili ya kufahamu kero zao na kuzipatia ufumbuzi sambamba na kutangaza miradi iliyotekelezwa na Serikali kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja.