Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Kigoma
MTATHIMI Mwandamizi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rashid Mageta, amesema “disclosure” ni sehemu muhimu ya mchakato wa uthamini inayompa mwananchi fursa ya kushirikiana na mthamini katika kuhakiki taarifa za mali yake kabla ya mchakato kukamilika.
Kutokana na umuhimu huo ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma kutumia zoezi la kuhakiki taarifa za mali zao na kutoa maoni pale wanapoona kuna taarifa ambazo hazijaandikwa kwa usahihi katika mchakato wa uthamini.

Akizungumza mkoani humo Mageta amesema,zoezi hilo linampa mwananchi nafasi ya kuona taarifa zilizokusanywa kuhusu mali yake na kueleza endapo kuna jambo ambalo halijaakisi hali halisi, ili kuwezesha marekebisho kufanyika mapema pale hoja inapobainika kuwa na msingi.
Mageta amesema,utaratibu huo umewekwa kwa mujibu wa Kanuni Na. 64 za Uthamini na Usajili wa Wathamini, kwa lengo la kuhakikisha changamoto zinazoweza kujitokeza zinabainishwa na kushughulikiwa mapema.
Katika utekelezaji wa zoezi hilo mkoani Kigoma, jumla ya wananchi 886 wamepangwa kufikiwa kwa ajili ya zoezi la “disclosure”, ambapo hadi sasa wananchi 819,takribani asilimia 92.4, kutoka maeneo ya Masanga, Mungonya, Msufini na Butunga, wamefikiwa na kupata fursa ya kuhakiki taarifa zao za mali na fidia.
Aidha, wananchi 67, sawa na asilimia 7.6, ambao bado hawajafika kuhakiki taarifa zao, wamehimizwa kutumia fursa hiyo na kufika katika maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya “disclosure” ili kuhakiki taarifa zao na kutoa hoja mapema.
Ametoa wito kwa wananchi ambao bado hawajafika katika maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya disclosure kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kuhakiki taarifa zao na kutoa hoja mapema badala ya kusubiri mchakato wa uthamini kukamilika.



More Stories
Dkt.Homera awasili Wizara ya Nishati
Nimekuja kuiunganisha timu ya maendeleo si kutawala:Magomi
Waandishi wa Habari Tanzania, Oman waandika historia