Na Joyce Kasiki,Dodoma
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema ubunifu wa kiteknolojia ni nyenzo muhimu katika kuongeza tija, kuanzisha biashara mpya, kutengeneza ajira na kukuza uchumi, akisisitiza umuhimu wa kuwezesha kampuni changa za TEHAMA kupata mitaji ya kukuza shughuli zao.
Kairuki amesema hayo Oktoba 2, 2026, jijini Dodoma wakati akizindua programu ya kuwezesha mitaji kwa kampuni changa za TEHAMA (start-ups), ambayo inalenga kusaidia wabunifu kubadilisha mawazo na bunifu zao kuwa bidhaa, huduma na biashara zenye ushindani.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza ubunifu wa kiteknolojia kupitia taasisi mbalimbali, ikiwamo Tume ya TEHAMA na Tume ya Sayansi na Teknolojia, sambamba na kuimarisha ujuzi na uwezo wa kitaifa katika sekta hiyo.
“Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya kukuza ubunifu kupitia taasisi ikiwemo Tume ya TEHAMA na Tume ya Sayansi na Teknolojia, sambamba na kuimarisha ujuzi na uwezo wa kitaifa katika sekta hiyo,” amesema.
Kwa mujibu wa Kairuki, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka mkazo katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kama kichocheo cha kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa.
Amesema Serikali inalenga kuhakikisha mawazo ya Watanzania hayabaki kuwa mawazo pekee, bali yanapata mazingira ya kuyaendeleza na kuyabadilisha kuwa bidhaa, huduma au biashara zinazoweza kukua na hatimaye kuanzisha kampuni zenye ushindani katika soko la ndani na kimataifa.
Akizungumzia programu hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya TEHAMA, Dkt. Henry Mwanyika, amesema kampuni nyingi changa zimekuwa zikikwama katika hatua za awali kutokana na ukosefu wa mitaji, hali ambayo imekuwa ikipunguza uwezo wao wa kukua na kushindana katika soko.
Amesema ujio wa programu hiyo utasaidia kukabiliana na changamoto ya mitaji na kuwezesha kampuni changa kuendeleza shughuli zao pamoja na kuongeza uwezo wa kushindana ndani na nje ya nchi.
“Programu hii inaenda sambamba na dira ya Tume ya TEHAMA na Taifa ya 2050. Sisi kama Tume ni daraja la kuwasaidia vijana kabla na baada ya kuanzisha biashara, hivyo programu hii itasaidia kukuza uchumi na ajira kwa vijana,” amesema Mwanyika.
Amesisitiza kuwa fedha zinazotolewa kupitia programu hiyo ni mikopo, si ruzuku, hivyo wanufaika wanatakiwa kuzitumia kwa tija na kuzirejesha ili kuwezesha kampuni nyingine changa kupata fursa hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Status Association, Zahoro Muhaji, amesema takribani Sh trilioni moja zimeelekezwa katika uwekezaji kwenye kampuni changa za TEHAMA nchini Tanzania tangu mwaka 2021.
Amesema uwekezaji huo umeendelea kuchochea ukuaji wa sekta ya teknolojia na kufungua fursa zaidi kwa vijana na wabunifu wa teknolojia.
“Mitaji tunayopewa kupitia programu hii si sadaka wala ruzuku, hivyo wanufaika tunapaswa kuhakikisha inatumika kwa tija na kurejeshwa ili kutoa fursa kwa kampuni nyingine changa kunufaika,” amesema Muhaji.

More Stories
Itunda: Vikundi 170 vyafaidika zabuni za asilimia 30
Utalii wa Arusha wanusa fursa mkutano wa IPU
Wachimbaji wadogo Geita wapatiwa leseni tatu mpya