Judith Ferdinand, TimesMajira Online
Wananchi wa Kata ya Kayenze iliopo wilayani Ilemela mkoani Mwanza,wameondokana na adha ya kufuata huduma za afya umbali mrefu huku wakiomba serikali kuwasaidia sehemu ya kuhifadhia maiti(mochwari).
Hiyo ni baada ya kata hiyo kupokea kiasi cha milioni 250,fedha zilizotoka serikali kuu kupitia tozo za miala ya simu ambayo imetumika katika ujenzi wa kituo cha afya Kayenze
ambacho kinatarajia kuhudumia wananchi zaidi ya 20,000 na kuwapunguzia adha ya kufuata huduma za afya mbali.
Wakizungumza katika uzinduzi wa kituo cha Afya Kayenze kilichozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,wananchi wa Kata hiyo akiwemo Diwani wa Kata ya Kayenze Issa Dida,amesema kata hiyo imepatiwa kiasi cha milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Kayenze ambacho ni muhimu sana kwa wananchi wa kata hiyo yenye kaya zaidi ya 3,000.
Dida amesema, awali ili kuwa changamoto kwa wakazi wa kata hiyo kupata huduma za afya kwani walikuwa wanatumia gharama kubwa na umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma hiyo katika kituo cha afya kata jirani.
” Kata hii ina kaya 3,225 na wakazi zaidi 18,000,hivyo zaidi ya watu 20,000 ikiwemo wa kata jirani wanahitaji kutumia kituo hiki, tunaishukuru serikali kutupatia kituo hiki ambacho kilikuwa ni hitaji maalumu kwa wakazi wa Kayenze,”amesema Dida.
Pia amesema,kwa sasa uhitaji mkubwa walionao wananchi wa kata hiyo ni jengo la kuhifadhia maiti kwani huduma hiyo wanaifuata katika kituo cha afya Karume kilichopo Kata ya Bugogwa.
Ambapo kuusafirisha mwili kuutoa Kayenze mpaka kituo cha afya Karume unagharimu kiasi cha shilingi 80,000 hadi 100,000,hapo bado gharama za kuhifadhia maiti.
“Sehemu ya kuhifadhia maiti ni hitaji kubwa ambalo tunahitaji kupata, tunamshukuru Rais kwa awamu ya kwanza ya kutupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituoa hiki,hivyo tunuomba angalau atupatie awamu ya pili ili tuweze kujenga wodi za wagonjwa na vitu vingine,”.
Mmoja wa wakazi wa Kayenze Hawa Omari,amesema kupitia kituo hicho wanakayenze kwa sasa hivi wanatakiwa wapate huduma za kimatibabu,wakina mama wajawazito wajifungulie hapa pia wanaomba na wodi ili watu wawe wanalazwa hapo hapo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Dkt.Charles Samson,amesema,katika kituo hicho cha afya Kayenze wamejenga jengo la OPD, maabara pamoja na sehemu ya kuchomea taka na maseptenki.
Dkt.Samson amesema,wamejenga kituo cha afya katika kata hiyo kwa sababu ya wingi wa watu hivyo wameona ni muhimu kwa ukanda huo kusogezewa huduma hiyo ya afya karibu ambao una wavuvi wengi na wanazaliana sana huku vifo vya kina mama vipo juu.
“Kwaio tukipata fedha nyingine milioni 250, tutaongeza majengo mengine kama ya upasuaji ili kuwanusuru ndugu zetu,vifo vya uzazi na watoto wachanga pamoja na kuwapunguzia umbali wa kufuata huduma hiyo,”amesema Dkt. Samson.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Modest Apolinary,amesema ujenzi huo umetumia miezi mitatu na sasa umekamilika na huduma zimeanza kutolewa siku tatu zilizopita.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masalla,amesema Kayenze ni kata ambayo ipo pembezoni mwa mji na inachangamoto kadhaa ambapo kwa Sasa inaenda kupata sifa kama maeneo mengine ya kata 19 zilizopo wilayani Ilemela.
“Leo tunakuwa wa kwanza kukabidhi kituo cha afya ambacho tumekijenga kwa siku 90,ambao tumeweza kutokana na ushirikiano kati ya viongozi,watendaji na wananchi,tulipatiwa fedha tukiwa tumechelewa tofauti na maeneo mengine ambao walipatiwa fedha mwezi Agousti huku sisi tukipokea mwezi Oktoba,” amesema Masalla.
Awali akizungumza baada ya kuzindua kituo hicho cha afya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel, amesema siku chache zilizopita katika utaratibu wa Rais aliupatia Mkoa wa Mwanza fedha kwa ajili ya kujenga vituo 10 vya afya ikiwemo hicho cha Kayenze ambacho kilikuwa cha mwisho kupatiwa fedha.
Mhandisi Gabriel amesema,ameridhishwa na kazi nzuri iliofanywa huku mahitaji machache yaliyobakia katika kituo hicho anasubilia barua aipeleke ili aseme mradi umekamilika ili aombe fedha kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya mama na mtoto na baadae wataona namna ya kujenga majengo mengine.
“Ilemela mmekuwa wa kwanza tena kumaliza mradi kwa wakati,niwapongeze kwani siyo jambo jepesi,fanyeni utafiti kujua siri ya mafanikio yenu na kulinda umoja wenu ili kujenga Ilemela mpya, wengine wanajua fedha zikija ni za kujinufaisha binafsi wakati ni za umma,mzidi kushikamana na mtangulize maslahi ya nchi mbele kwa kuwa na uwazi na uwajibikaji kwenye fedha za umma,”amesema Mhandisi Gabriel.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kituo cha afya Kayenze ambacho kimejengwa kupitia fedha za tozo za miala ya simu zilizotolewa na serikali kuu ambacho kimegharimu kiasi cha milioni 250
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi