July 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Katavi watakiwa kutumia uhuru wa kujieeza kwa maendeleo

Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi

Wananchi wa Mkoa wa Katavi wameombwa kutumia uhuru wa kujieleza kama nyenzo muhimu ya kuchochea maendeleo ya nchi.

Maendeleo ambayo yatapatikana kupitia uhuru wa watu kutoa maoni yenye kuleta uwajibikaji sio kwa serikali pekee bali jamii yote kwenye kuibua mahitaji ya wananchi na kufuatilia utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maendeleo.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi Nahemia James, amesema hayo Julai 02, 2024 Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda wakati akizinduzi semina ya kijamii ya siku moja kuhusu uhuru wa kujieleza unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya ABAROLI na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania(UTPC).

Kaimu Katibu Tawala huyo ameeleza kuwa jamii ikitumia uhuru wa kujieleza inapaswa kufuata misingi ya kisheria,kuongozwa na uzalendo na haki pasipo kukiuka tamaduni,mila na desturi za nchi ambazo zimekuwa nguvu ya umoja na mshikamano wa Watanzania.

“Waandishi wa haba mnapaswa kuzingatia weledi kwenye kazi zenu za kuhabarisha umma kama sehemu yenu ya uhuru wa kujieleza na mfahamu nyie ni kiungo kati ya serikali na jamii,”amesema James.

Rais wa UTPC Deogratius Nsokolo amesema kuwa uhuru wa kujieleza unatoa nafasi kwa wananchi kuwa na uwezo wa kuhoji na kutoa matatizo yanayoikabili jamii ili wenye mamlaka waweze kuchukua hatua ya kutatua.

Pia amefafanua kuwa jamii inakabiliwa na matatizo ya ukosefu wa maji safi, ukatili wa aina mbalimbali kama vile ubakaji na unyanyasaji kwa watoto na wanawake,ubadhilifu wa miradi ya maendeleo ambayo serikali inatumia fedha nyingi kuijenga ambapo yote hayo yatakoma endapo wananchi watatumia uhuru wa kujieleza kufichua hali hiyo.

“Nitoe wito kwa wanahabari kushuka katika jamii kuandika habari zinazowagusa na kuepuka mara nyingi kuandika habari za viongozi pekee,”amesema Nsokolo.

Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC Keneth Simbaya amefafanua dhima ya uhuru wa kujieleza unaenda sanjari na utekelezaji wa 4Rs za Rais Samia Suluhu Hassan ambazo ni Maridhiano (Reconciliation), Mabadiliko (Reforms), ustahimilivu (Resilience) na kujenga upya (Rebuilding)

4Rs ni msingi imara zaidi kwenye ujenzi wa taifa ambalo lina uhuru wa kujieleza hususani katika kuchochea ustawi wa maendeleo ya watu ambao Rais Samia unausisitiza kila mahala.

Mkurugenzi huyo ameeleza Katiba ya Jamuhuri ya Muugano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayofanyiwa marekebisho mara kwa mara Ibara ya 18 inatoa mambo makuu matatu kuhusu uhuru wa kujieleza.

“Msingi wa Ibara ya 18 unatoa haki ya kujieleza kwenye kutafuta taarifa,kupata taarifa na kutoa taarifa” amesema Keneth akisisitiza kuwa taarifa hizo zinapaswa mtu mwingine kuzitoa.

Keneth amefafanua “Mtaanza kuona kwamba hakuna njia ya kuweza kuepuka suala la kutumia uhuru wa kujieleza hivyo kama utakuwa hautafuti utapaswa kutoa hizo taarifa ili wengine waweze kupata hizo taarifa na waitumie kwenye mambo mbalimbali,”.

Kuhusu mipaka ya uhuru ya kujieleza amesema kuwa kisheria mipaka hiyo lazima iwe imehakikiwa kwenye mipaka ya misingi ya haki na mipaka hiyo itakuwa imepimwa kisheria.


Katika hatua nyingine amewataka Waandishi wa Habari kutenga muda wa kukaa na wadau wa habari kama nyenzo ya kuweza kukosolewa mahala walipokosea nani wapi wanapaswa kuboresha na wapi wamefanya vizuri kwani vinawajibika kwa jamii.

Amesema kuwa kitendo hicho kitaweza kuinua imani ya wananchi kwa Waandishi wa Habari ambayo imeanza kupotea kwa sababu ya kuacha kufuata misingi ya taaluma ya uandishi wa habari na kuandika habari za wanasiasa huku zikiachwa habari za baadhi ya hosptali kukosa madawa.

Mwenyekiti wa Taasisi ya shirikisho la watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA) Mkoa wa Katavi Anna Nchagwa, ameiomba serikali kujenga miundombuni rafiki ambayo itawawezesha watu wenye ulemavu kutoa maoni yao.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa watu wenye ulemavu wanauwezo wa kutoa mchango wa maoni kwa maendeleo ya taifa lao kwa kuwa wanauwezo mkubwa wa kutumia uhuru wa kujieleza kama watapewa nafasi shiriki sawa na watu wengine.