January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi kata ya sangambi kunufainika na kituo kipya cha afya

Na Esther  Macha,TimesMajira Online, Chunya
ZAIDI ya wakazi 10000 wa Kata ya Sangambi,  wilayani Chunya katika Mkoa wa Mbeya, wanatarajiwa kupata huduma za Afya baada ya serikali kutoa sh milioni 316 kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya  kwenye Kata hiyo.

Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Ntundu Chapa alipozungumza na timu ya waandishi wa habari wa mkoa wa Mbeya  juzi amesema kwa  sasa ujenzi wa kituo hicho cha Afya umekamilika kwa asilimia 85 na kwamba huduma za matibabu zinatarajiwa kuanza Juni mosi mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Chunya , Tamimu Kambona amesema maelekezo  ya serikali kuwa kila halmashauri inayokusanya mapato  ya ndani ya Bil.3 mpaka  bil.4 iweze kujenga kituo cha afya kimoja  lakini halmshauri  hiyo  iliamua katika vikao vyake  kujenga kituo cha afya kimoja na  pamoja na madarasa mawili kwa kutumia mapato ya ndani .

Akizungumza na timu ya waandishi wa habari waliotembelea eneo la kituo hicho afya cha Sangambi Kambona  amesema kuwa mpaka sasa wametumia shilingi million.300 ambazo zinatokana na mapato ya ndani na kuwa sasa wanaenda awamu nyingine ya mwisho ambapo wametenga mil.40  ambayo inaenda kumaliza ujenzi wa kituo hicho.

Aidha Kambona amesema kuwa  lengo la halmashauri kwa  sasa ni kumaliza majengo yote ili  kuweza kuwahamisha watumishi kutoka kituo cha zamani kituo hicho kianze kufanya kazi haraka ili kuwasaidia wananchi  kupata matibabu.

“Kituo hiki tunarajia kianze kufanya kazi mwezi wa sita mwaka huu waanze kutoa huduma,lakini vifaa tiba vyote vitakuwepo  kutokana na zahanati ya awali ambayo inaendelea kufanya kazi mpaka sasa wakati wananchi wakiendelea kusubiri kukamilika kituo hicho cha afya na kuwa bajeti ya mwezi wa saba wametenga kiasi cha fedha ili kuweza kununua vifaa tiba vingine vikiwemo vitanda vya wagonjwa”amesema Kambona.

Mkazi wa Sangambi Wilayani Chunya ,Fatuma Juma amesema kuwa  hospitali ipo moja tu  na kuwa huduma bado ni changa na haijaweza kuboreshwa vizuri .

Venance Mwambugi Mkazi wa Sangambi amesema wanashukuru ujenzi wa kituo  cha afya kinaelekea ukingoni kukamilika kwani siku za nyuma  walikuwa na zahanti ambayo ni ndogo  hasa ukizingatia kata hiyo ina vitongoji vingi ambavyo vyote vinategemea zahanati hiyo na akina mama wajawazito walikuwa wanaenda kujifungulia hospitali ya wilaya Chunya kutokana na zahanati hiyo kuwa ndogo .

Mwambugi amesema  wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan  kwa kuwasaidia kujenga kituo cha afya hivyo waliomba kituo hicho cha kukamilika mapema ili wananchi waweze kupata matibabu na akina mama wajawazito waweze kujifungulia katika kituo hicho cha afya badala ya kusafiri umbali mrefu.

Baadhi ya waabdishi wa habari wakiwa picha ya pamoja na mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Chunya Tamimu Kambona