November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Kata ya Rukoma washukuru kujengewa sekondari

Na Ashura Jumapili, TimesMajira,Online, Bukoba

WAKAZI wa Kata ya Rukoma katika halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, wameiomba Serikali kukamilisha haraka usajili wa shule ya sekondari Rukoma, ili kuwaepusha watoto wao kutembea umbali wa kati ya kilomita saba hadi 18 kwenda kusoma katika shule ya sekondari Rubale, kutokana na kata yao kutokuwa na shule.

Wakizungumza katika mkutano maalumu wa hadhara ulioitishwa na diwani wa kata hiyo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Murshid Ngeze, baadhi ya wananchi akiwamo, Idaya Omary walisema watoto wao wameteseka kwa muda mrefu kwenda kufuata elimu mbali na kata yao.

Omary alisema wamepata faraja kwa kujengewa shule karibu. “Tunawashukuru viongozi wetu kutujengea shule tumefarijika sana, tumeambiwa usajili wake bado haujakamilika, ombi letu kwao watusaidie kukamilisha haraka maana watoto wetu wamekuwa wakiteseka kwenda shule ya sekondari Rubale.

Shule hiyo ipo mbali kiasi kwamba watoto wakitoka shule jioni wanakuwa wamechoka wanaishia kulala hawawei tena kujisomea,” alisema.

Wananchi wa kata ya Rukoma wakimsikiliza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukoba, Murshid Ngeze ambaye ni diwani wa kata hiyo kuhusiana na kukamilika kwa sekondari mpya ya Rukoma.

Naye Najiath Shaban alisema mbali na watoto wa kike kubeba mimba na wengine wa kiume kuacha shule kutokana na shule kuwa mbali, pia baadhi ya wazazi waliwalazimisha watoto wao wafanye vibaya katika mitihani yao ya kuhitimu darasa la saba, ili wasiendelee na masomo ya sekondari.

“Kutokana na umbali mrefu na baadhi ya wazazi kutokuwa na fedha za kuwanunulia baiskeli watoto ili ziwasaidie kwenda shule, kuna wazazi waliwambia watoto wao wasifanye vizuri katika mitihani hata kama walikuwa na uwezo wa kufanya mitihani na kushinda, tatizo hili linatokana na shule wanakopelekwa kuwa mbali mno,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Murshid Ngeze, alisema yeye na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo wanakwenda kukamilisha usajili wa shule hiyo ili Januari mwakani watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika kata hiyo, waanze masomo.

Majengo ya madarasa

“Kwa sasa madarasa yapo na mchakato wa kukamilisha usajili unaendelea, hakuna tena haja ya watoto kuwaacha wateseke kwenda shule ya sekondari Rubale, tutahakikisha Januari wote wanaanza masomo hapa Rukoma sekondari, nawaahidi hilo,” alisema Ngeze.

Pia Mwenyekiti huyo wa halmashauri alisema kuwa wamepata fedha nyingine sh. milioni 470 kwa ajili ya kujenga madarasa mengine manane, jengo la utawala, maabara tatu na matundu 20 ya vyoo katika shule hiyo, na kwamba kufikia Februari, mwaka huu vitu vyote hivyo vitakuwa vimekamilika na kuwezesha kuwepo kwa madarasa ya kutosha.

Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara ofisa elimu wa kata hiyo, Dankan Byobangila, alisema walipata fedha za Uviko 19 kiasi cha sh. milioni 60 kwa ajili ya kujenga vyumba vitatu vya madarasa na kutengeneza madawati 150, ambavyo tayari vimekamilika.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukoba, Murshid Ngeze ambaye ni diwani wa kata hiyo akizungumza na wananchi kuhusiana na kukamilika kwa sekondari mpya ya Rukoma.

Byobangila alisema wananchi walijitolea nguvu zao na kuchanga sh. milioni 42 na halmashauri ikatoa sh. milioni 25 na kufikisha jumla ya sh. milioni 67 zilizotumika kujenga vyumba vingine vitatu, na kufanya shule hiyo mpya kuwa na jumla ya vyumba vya madarasa sita, ambavyo wanatarajia kuvitumia kupokea wanafunzi 225 waliofaulu kutoka katika kata hiyo.

Alisema kuwa katika shule sita za msingi zilizoko katika kata hiyo, watainiwa waliofanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka huu walikuwa ni 295 na kati ya hao watoto 225 walifaulu, ambao ni sawa na  asilimia 85 ya waliofanya mtihani.