December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Kasulu wamshukuru Rais Samia kumaliza kero ya wanafunzi

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Kasulu

WAKAZI wa Vijiji vya Kagerankanda na Mvinza vilivyoko katika kata ya Kagerankanda Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wamemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea shule ya msingi katika kila kijiji ili kumaliza msongamano wa watoto shuleni.ù

Wametoa shukrani hizo juzi walipokuwa wakiongea na mwandishi wa gazeti hili aliyefika katika kata hiyo kujionea hali ya miundombinu ya Elimu.

Abdul Mihezagiro (50) mkulima, mkazi wa Kijiji cha Mvinza amesema awali kata hiyo ilikuwa na shule moja tu iliyokuwa kwenye Makao Makuu ya kata, Kijiji cha Kagerankanda hali iliyopelekea watoto wanaotoka Kijiji cha Mvinza kutembea umbali mrefu sana kwenda na kurudi shuleni.

Amebainisha kuwa umbali huo ulifanya watoto wengi kushindwa kuendelea na masomo huku wengine wakiishia vichakani na kurudi nyumbani.

Aidha ameongeza kuwa baadhi ya watoto wa kike walishindwa kumaliza shule kwa kupata ujauzito huku wengine wakitoroshwa na wanaume.

‘Tunamshukuru sana Rais Samia kwa kutujengea shule katika kila kijiji na sasa amepanua wigo zaidi kwa kutuongezea shule katika Kitongoji cha Songambele kilichoko katika Kijiji cha Mvinza’, amesema.

Mwalimu Nocodemus Kibona wa shule ya msingi Mvinza amempongeza Rais Samia kwa kuipatia halmashauri ya wilaya hiyo zaidi ya sh mil 360 kwa ajili ya ujenzi wa shule nyingine katika Kitongoji cha Songambele ambao utaifanya kata hiyo sasa kuwa na shule tatu hivyo kumaliza kwa kiasi kikubwa msongamano wa wanafunzi katika shule mama ya Mvinza kama alivyofanya kwa shule mama ya Kagerankanda.

Amefafanua kuwa awali shule mama ya Kagerankanda ilikuwa na watoto zaidi ya 2000 serikali ikawajengea shule ya Mvinza na sasa shule hiyo imefikisha watoto 2186 wa darasa la 1-7 hivyo shule hiyo mpya itasaidia sana kupunguza msongamano huo.

Akizungumza miradi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Joseph Kashushura amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia halmashauri hiyo zaidi ya sh bil 2.5 katika mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023 kwa ajili ya kuboreshwa miundombinu ya shule za msingi na sekondari kiwemo kujengwa shule mpya.

Amebainisha kuwa maboresho hayo ni kichocheo kikubwa kwa watoto wa shule zote kufanya vizuri katika masomo yao hivyo kuongeza kiwango cha ufaulu na kupungua kwa vitendo vya utoro kama sio kwisha kabisa.