Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Handeni
WANANCHI wa Kijiji cha Kwedizinga, Kata ya Kwedizinga, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wamelishukuru Shirika la World Vision Tanzania, Mkumburu Area Programme kwa kuwawezesha kupata mradi wa maji.
Kwani mradi huo uliotekelezwa kwa ufadhili wa World Vision Tanzania, na Taasisi ya We Are Water Foundation kutoka nchini Hispania, utawezesha wananchi 4,486 kufaidika na maji hayo, na kuwaondolea adha ya muda mrefu kuchota maji kwenye vidimbwi, tena usiku wa manane na kuhatarisha maisha yao.
Waliyasema hayo Novemba 4, 2024 wakati wanazungumza na waandishi wa habari mara baada ya uzinduzi wa mradi huo uliofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Wakili Albert Msando kwenye Kijiji cha Kwedizinga.
“Mradi huu umeleta neema na faraja kwa wananchi wa Kijiji cha Kwedizinga, kwani ukiacha wananchi kuchota maji kwenye vidimbwi, pia iliwalazimu kwenda umbali mrefu kufuata maji hayo, huku wakitembea usiku mwingi, na kuhatarisha maisha yao kwa kugongwa na nyoka, huku ndoa za wanawake zikiwa mashakani” alisema Venance Alberto mkazi wa Kijiji cha Kwedizinga.
Naye Richard Mgaya wa kijiji hicho, alisema kwa kupata mradi huo wa maji kutawapunguzia wananchi gharama ya kununua maji, kwani ukiacha wananchi waliokuwa wanakwenda porini kutafuta maji kwenye vidimbwi, baadhi ya wananchi walikuwa wananunua maji kwenye boza ndoo moja ya lita 20 kwa sh. 1,000, lakini kwa sasa watanunua ndoo hiyo kwa sh. 50 tu.
Muuguzi wa Afya Zahanati ya Kwedizinga Hadija Masimba alisema maji hayo ambayo pia yamefika Shule ya Sekondari Kwedizinga na Zahanati ya Kwedizinga, yatawasaidia kuepukana na magonjwa ya mlipuko, kwani watu watajisaidia na kuweza kunawa mikono. Lakini kwa ajili ya akina mama wanaojifungua, maji hayo ni muhimu sana kwao kwa ajili ya kuweza kukaa sawa.
Naye mwanafunzi Shania Shaaban (17) ambaye alisaidia kupata mradi huo wa maji, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa akiwa kidato cha pili Shule ya Sekondari Kwedizinga mwaka 2022, Shirika la World Vision lilimuwezesha kushiriki Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (Cop27, Egypt2022), na akiwa kule alitumia fursa hiyo kuwapata wadau Taasisi ya We Are Water Foundation.
“Nilikutana na We Are Water Foundation kupitia Carlos, nikamueleza shule ninayosoma na kijiji changu ninapotoka kuna shida kubwa sana ya maji. Hivyo, walinielewa, na wakaweza kufika nchini na kuweza kushirikiana na World Vision na kuweza kutuletea mradi huu wa maji” alisema Shania ambaye mwaka huu amemaliza kidato cha nne kwenye shule hiyo, na anasubiri majibu.
Shania alisema shuleni kwao kulkuwa na Club ya Mazingira ambayo ilimfanya apate nafasi ya kwenda Misri kwa ufadhili wa World Vision, ambapo kabla ya kwenda alifanyiwa usaili na kuelezea jinsi uharibifu wa mazingira unavyotokea katika jamii yao, na ndipo alipopata nafasi ya kuelezea kuhusu mazingira, na kuchaguliwa kwenda Misri.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Mratibu wa Mkumburu AP Daniel Chuma alisema uliibuliwa na wanajamii wenyewe kutokana na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama, na utekelezaji wake ulianza mwaka 2023-.2024.
“Mradi huu wa usambazaji maji katika Kijiji cha Kwedizinga umetekelezwa katika awamu moja kwa hatua mbili kwa kutumia Wakandarasi wawili. Wanufaika wa moja kwa moja ni wananchi 3,890, na wanufaika wasio wa moja kwa moja ni 596, hivyo jumla kuwa wananchi 4,486” alisema Chuma.
Chuma alisema mradi huo uliogharimu sh. 245,886,900 ni wa kisima kirefu, na umejengewa tenki la lita za ujazo 50,000, mabomba ya usambazaji maji yenye urefu wa kilomita 4.3, vilula 10, ujenzi wa pump house, ununuzi wa Solar kwa ajili ya kusukuma maji.
Amesema Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Handeni walichangia ufundi na usimamizi, uandaaji wa michoro na makisio, na ushauri na usimamizi wa kiufundi, wakati kwa upande wa jamii ni kutenga na kutoa maeneo kwa ajili ya mradi, usimamizi wa mradi, na ulinzi wa vifaa na miundombinu.
Mwakilishi wa We Are Water Foundation Carlos Garriga kutoka Hispania alisema wamefurahi kutoa huduma kwa jamii baada ya kuombwa kufanya hivyo na mwanafunzi Shania baada ya kukutana nae kwenye Mkutano wa Mazingira, Misri, na ameomba mradi huo uwe endelevu, na kutaka maji yafike na kutumika kwa walengwa waliokusudiwa ikiwemo wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kwedizinga, ambapo tayari World Vision wamefikisha maji hayo.
Mkuu wa Wilaya, Msando alisema mradi huo umeongeza kiwango cha upatikanaji maji kwenye wilaya hiyo na kufikia asilimia 42. Lengo la Serikali ni kufikisha asilimia 85 ya upatikanaji maji vijijini ifikapo 2025, hivyo amewataka wananchi kulinda mradi huo hasa miundombinu yake ili uwe endelevu, kwani wanapopata miradi ya maji kupitia wadau hao, inawaongezea kiwango cha upatikanaji maji.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais