November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi 5,621 kunufaika na mradi wa maji Mayo, Bumbuli

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Bumbuli

WANANCHI 5,621 wa vijiji vya Kizanda na Mayo, Kata ya Mayo, Halmashauri ya Bumbuli, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wanatarajia kunufaika na mradi wa maji wa Mayo.

Hayo yamesemwa Juni 13, 2023 na Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim alipofika kukagua na kufungua mradi huo.

Mhandisi Sizinga amesema ujenzi wa miundombinu ya maji katika mradi huo ni miongoni mwa miradi ya maji iliyokamilka ambayo inatekelezwa na Ofisi ya Meneja RUWASA Lushoto kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdallah Shaib Kaim (katikati) akifungua koki kwenye Mradi wa Maji Mayo. Wengine ni Waziri wa Nishati na Mbunge wa Jimbo la Bumbuli January Makamba (wa pili kulia), Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro (wa pili kushoto), Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Lushoto Ali Daffa (kushoto).

Amesema mradi huo uliwekewa jiwe la msingi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2022, na ulitekelezwa na Mkandarasi Mbesso Construction Co. Ltd wa Dar es Salaam kwa mkataba ulioanza utekelezaji wake Februari Mosi, 2022 na kukamilika Septemba 30, 2022.

Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga,Waziri wa Nishati January Makamba (wa pili kulia) akimtwisha ndoo mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari Mayo, mara baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdallah Shaib Kaim kufungua mradi wa maji Mayo.

“Utekelezaji wa mradi umekamilika kwa asilimia 100 kulingana na mkataba, na unategemea kunufaisha wakazi 5,621 wanaoishi kwenye vijiji vya Kizanda na Mayo na umegharimu zaidi ya milioni 430(430,909,580) ambazo ni gharama za mkandarasi katika ujenzi wa miundombinu, na amelipwa fedha zote,” amesema Sizinga.

Sizinga amesema kazi zilizofanyika kwenye mradi huo ni chanzo kipya cha maji, ufyekaji wa njia za bomba kuu, tenki la maji lenye ujazo wa lita 90,000, vituo vya kuchotea maji (vilula) vinane, vituo saba vya nyongeza, uchimbaji wa mitaro ya bomba yenye urefu wa mita 15,000, ulazaji na uungaji mabomba mita 15,500, ujenzi wa chemba pamoja na vifaa vyake, ujenzi wa BTP.

“RUWASA tunatoa shukrani za dhati kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupatia fedha za miradi ya maendeleo,tutazisimamia vizuri ili ziweze kuleta tija kwa wananchi na kufikia malengo yaliyokusudiwa,”amesema Sizinga.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdallah Shaib Kaim (kulia) akipata maelezo ya namna mradi wa maji Mayo ulivyojengwa kutoka kwa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga (kushoto),wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro.

Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim ameupongeza mradi huo ambapo amesema umejengwa kwa viwango, na utanufaisha wananchi wengi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro alimshukuru Rais Dkt. Samia kwa miradi mingi inayotekelezwa kwenye wilaya hiyo ikiwemo miradi ya maji.

Mbunge wa Jimbo la Bumbuli,Waziri wa Nishati January Makamba amewaeleza wananchi wa Jimbo hilo kuwa barabara ya kutoka Soni- Bumbuli- Dindira- Kwashemshi- Old Korogwe ya kilomita 73, inaanza ujenzi wake mwaka huu kwa kiwango cha lami.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Mayo wakimsikiliza Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdallah Shaib Kaim (hayupo pichani) wakati alipofika kufungua mradi wa maji Mayo.