December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi 2,521 Majani Mapana waondokana na adha ya maji

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online, Handeni

Wananchi wa Kijiji cha Majani Mapana, Kata ya Kabuku Ndani, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wameondokana na shida ya maji baada ya kukamilika kwa mradi wa maji Majani Mapana.

Lengo la mradi huo ni kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji hicho wapatao 2,521.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM) Mhandisi Yohana Mgaza kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim alipofika kufungua mradi huo ambao umekamilika kwa asilimia 100.

Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim akimtwisha ndoo mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Majani Mapana mara baada ya kuweka jiwe la ufunguzi wa mradi wa maji Majani Mapana, Kata ya Kabuku Ndani, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Amesema Majani Mapana ni moja kati ya vijiji vilivyopo katika Kata ya Kabuku Ndani katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni,kijiji kilipata ufadhili wa kujengewa mradi wa maji kupitia fedha za UVIKO-19, kwa usimamizi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main.

Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Saxon Building Contractors Ltd kwa mkataba Na. AE/093/2021-2022/W/01 na ulianza kutekelezwa rasmi mnamo Novemba 17, 2021 na ulikamilika Septemba 15, 2022.

“Lengo la mradi huu ni kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Kijiji cha Majani Mapana wapatao 2,521, umegharimu kiasi cha zaidi ya milioni 395 kati ya hizo, Serikali Kuu ni zaidi ya milioni 352 huku Wahisani zaidi ya milioni 38, ambapo Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira HTM zaidi ya milioni 18 na Comfort Aid International (Uchimbaji wa kisima) ni milioni 20 na wananchi ni milioni 5,”amesema Mhandisi Mgaza.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim (kulia) akiweka jiwe la ufunguzi wa mradi wa maji Majani Mapana, Kata ya Kabuku Ndani, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga kushoto ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Handeni Hashim Mgandilwa.

Mgaza amesema kazi zilizopangwa na kutekelezwa katika mradi huo ni pamoja na kuchimba kisima kirefu (Borehole), kujenga nyumba ya mitambo katika eneo la mijohoroni palipo na kisima, kujenga tenki la maji lenye ujazo wa lita 100,000 katika mnara wa mita sita, ujenzi wa jumla ya vituo tisa (vilula) vya kuchotea maji katika vitongoji vya Mikoroshini, Misufini, Mkulima, Ujamaa, Kibango na Kwamaluli.

Pia kuchimba na kulaza bomba kuu lenye urefu wa mita 2,622 kutoka katika kisima hadi katika tanki la maji,kuchimba na kulaza mabomba ya kusambazia maji yenye urefu wa jumla ya mita 3,777, kufunga pampu ya maji katika kisima kwa ajili ya kusukuma maji kwenda katika tanki, kufunga mfumo wa nishati ya jua (Solar) kwa ajili ya kuendeshea pampu ya maji na ujenzi wa Valve Chambers 12.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM) Mhandisi Yohana Mgaza akisoma taarifa ya mradi wa Majani Mapana kwa Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim alipofika kufungua mradi huo ambao umekamilika kwa asilimia 100.

“Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za mradi huu ambao utakwenda kutatua changamoto ya maji katika eneo letu na kufikia lengo la kumtua mama ndoo kichwani,”amesema Mhandisi Mgaza.