January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanakijiji Ledewa wataka huduma muhimu

Na David John, TimesMajira Online, Lipingu

WANANCHI wa Kijiji Cha Nindi kilichopo kata ya Lupingu wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, wamemuomba Mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga kusaidia upatikanaji wa huduma muhimu kama Zahanati, Umeme, Maji, pamoja na usafiri.

Kijiji hicho ambacho kina wakazi zaidi ya 2000 kinakabiliwa na changamoto hizo hususani ukosefu wa Zahanati hali inayosababisha wanawake kupata tabu wakati wakujifungua ambapo wanalazimika kusafiri umbali mrefu hadi Ludewa kufuata huduma hiyo.

Akizungumzia huduma hizo Editha Haule mkazi wa Kijiji cha Nindi amesema, hali ni mbaya kwao kama akina mama kwani wakati mwingine wanalazimika kujifungulia njiani kutokana na ukosefu wa usafiri lakini pia gharama nikubwa kutoka kijijini kwao hadi kufika wilayani Ludewa.

“Ki ukweli tunashukuru sana kumpata Kamonga kwani tunaamini atatusaidia, kutoka hapa kijijini hadi Ludewa ni shilingi 10, 000, hali inayosababisha wananchi kupata tabu. Hivyo tunamuomba Mbunge wetu atusaidie kutatua changamoto hizi mara tu atakapoapishwa,”amesema Editha.

Mkazi mwingine Leo Honjo maalufu (Mifwa) amesema, katika Kijiji Cha Nindi kina vitongoji vinne ambavyo ni Nindi Juu, Nindi Kati, Ipombo, Njelela lakini changamoto kubwa ni maji, umeme ambapo wanalazimika kufuata maji zaidi ya kilometa 15.

Amesema, akina mama wanazalia hadi njiani kutokana na usafiri, ukosefu wa Zahanati na kwamba ikitokea mwanamama amezalia njiani anatozwa faini ya shilingi 50,000, jambo ambalo linawagharimu Sana.

Kwaupande wake Anthony Haule, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nindi amesema jambo kubwa ambalo wanataka Mbunge awasaidie ni upatikanaji umeme wa uhakika ambapo kwa sasa umefika, lakini bado wananchi kuunganishiwa. Pia kuna tatizo la maji kwani akina mama wanatembea zaidi ya kilometa 15 kufuata huduma hiyo na kuleta kugomvi majumbani.

“Hapa wananchi wangu hawana shida kabisa kwani watampa kura zote Rais Dkt. John Magufuli kura zote na Diwani John Sikanda na Mbunge amepita bila kupingwa. Tunaamini atatusaidia sana na tunamuombea sana Mungu ambariki,”amesema Haule.

Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ludewa Stanley Kolimba akimnadi mgombea wa CCM Rais Magufuli na Diwani Sikanda amesema,Magufuli ni mbunifu, mchapa kazi, hivyo wampe kura zote za ndio na wahakikishe wachague mafiga matatu ili waweze kuwatumikia vizuri wananchi.

Akihutubia mbele ya wananchi waliojitokeza kusikiliza mkutano wa Mbunge uliofanyika katika viwanja vya Kanisa Katoriki Kamonga amesema, anahistoria na Kijiji Cha Nindi hivyo anawashukuru na anahakika watashirikiana pamoja.

Amesema, yeye hawezi kujivuna kama ni Bora kuliko wengine japo kuwa amepita bila kupingwa nakwamba anachoamini Mungu yuko pamoja na wananchi hao na kubwa zaidi anapita kumuombea kura Rais Dkt John Magufuli.

“Ndugu zangu nawaomba Siku ya Oktoba 28 kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kumchagua Dkt. Magufuli kiongozi ambaye ana Mungu, anafanya mengine kwa ajili ya Ludewa, Lupingu, Nindi. Hivyo lazima muonyeshe upendo kwake,”amesema Kamonga.

Kamonga amesema, zaidi ya bilioni 167 zimezama ili kutengeneza barabara kutoka Ludewa kwenda Njombe na Bilioni 66 kwa ajili ya elimu bila malipo na Bilioni tano kwa ajili miundombinu, hivyo hakuna sababu ya kushindwa kumpa kura na zaidi Rais atakarabati bandari za Lupingu na Manda ili Meli ziweze kuingia bandarini. Huku akiwataka wananchi kumchagua Diwani wa kata hiyo John Sikanda ili aendelee kuwatumikia.

%%%%%%%%%%%%