November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanakijiji cha Mdimni walivyochukua hatua kurudisha misitu ya mikoko iliyokauka

Na Penina Malundo, timesmajira

MABADILIKO ya tabiachi ni miongoni mwa athari kubwa za mazingira zilizoikumba kwa kasi dunia katika miaka ya karibuni, Mdimni kikiwa ni miongoni mwa vijiji vilivyoathiriwa na hali hiyo kati ya mwaka 2019 hadi 2020.

Athari zilizotokana na mabadiliko ya tabianchi, mwaka huo zilisababisha mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha madhara ya kimazingira miongoni mwayo ikiwa ni pamoja na kuanguka kwa miti mingi ya mikoko na kuyafanya maji ya bahari kuanza kufika katika maeneo ya makazi ya watu.

Wakazi wa kijiji hicho walizungumzia athari hizo, huku wakitaja hali waliyokumbana nayo kipindi hicho kabla ya kuchukua hatua yalikuwa magumu kiuchumi na kijamii kutokana na mabadiliko ya tabiachi.

Said Msati, aliyehama kijijini hapo mwaka 2020 na kuhamia kijiji jirani kwa sababu ya athari ya mabadiliko hayo anasema awali alikuwa anajua mvua inayonyesha ilikuwa ya kawaida, lakini baada ya muda mrefu ilianza kusababisha madhara mbalimbali ndipo alipogundua kuwa ilikuwa ni mvua kubwa na yenye madhara.

Msati anasema kazi yake kubwa ilikuwa kilimo, hivyo maji ya mvua yalipoanza kuongezeka jirani na makazi yake aliamua kuacha shughuli hiyo na nyumba yake baada ya miti ya mikoko kuanguka na maji kuzidi kusogea.

“Nilipoona tu hali hii inazidi na kuanza kubadilika shamba langu kujaa maji na mazao yangu  niliyoyapata kama Mpunga na Mihongo kuanza  kuharibika nilijua tayari mabadiliko ya tabianchi wanayosema yameingia katika kijiji chetu na kuhamua kuhama,” anasema.

“Maji yalianza kukata mitaa na kuanza kuingia katika nyumba zetu hali hii ilitutisha zaidi na kutufanya kuondoka kabisa maeneo hayo.”

Anasema hali hiyo ilimuathiri kiakili kutokana na kupoteza mazao yake aliyoyapanda kwa gharama na kutegemea kupata chakula yeye na familia yake pamoja na kuacha nyumba yake na kukimbia kijiji kingine.

Subira Khalid (sio jina lake halisi) anasema athari za mabadiliko hayo zilipoanza alijua ni jambo la kawaida, lakini alipoona madhara ya miti kuanguka na mingine kukauka nyakati za kiangazi akabaini kwamba athari za mabadiliko ya tabiachi zimewagusa.

Anasema nyumba zilizokuwa zipo karibu na fukwe za bahari zilianza kuathiriwa na upepo mkali ambao ulikuwa unapiga moja kwa moja katika nyumba hizo na nyingine kuezuliwa na upepo.

“Sitamani kukumbuka kipindi kile kwa kweli tulipata changamoto sana,maana ukikaa ndani ya nyumba unakuwa na hofu ya nyumba kuezuliwa na upepo hali iliyofanya wanakijiji wengi kuacha makazi yetu na kuhamia maeneo mengine,” anasema.

Naye Juma Cheka anasema watu walianza kuhama kijiji hicho kutokana na shughuli za kilimo na uvuvi kuanza kusumbua ambapo walikuwa hawajui kuwa ni athari za mabadiliko ya tabianchi yameanza.

Anasema watu wengi walikimbia kijiji hicho kutokana na misitu ya mikoko kuanguka na mingine kukauka,huku nyumba zikianza kuezuliwa na upepo  jambo lililoathiri shughuli za uvuvi na kukimbiza.

Cheka anasema wataalamu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) walienda kijijini hapo na kuwaambia kuwa athari hizo zilisababishwa na mabadiliko ya tabianchi, jambo lililoanza kuwajengea uelewa juu ya suala hilo.

***Wanakijiji cha Mdimni walivyochukua hatua kurudisha misitu ya mikoko iliyokauka

Mwenyekiti wa Kikundi cha Kimtaa, Maimuna Mkokwa ambao ndio walinzi wakuu wa Mikoko hiyo tangu kurejea kwa ikolojia yake, anasema kwa sasa wamekuwa wanaitunza mikoko hiyo ipasavyo kutokana na shughuli zao za ufugaji wa nyuki.

“Tulianza kuunda kikundi mwaka 2021 ambapo kikundi hicho kinakuwa na watu 18 kwa kila kikundi na tumeweza kupata elimu ya ufugaji wa nyuki katika misitu ya mikoko kutoka kwa wataalam wa mazingira na watu wa TFS,” anasema.

“Mikoko inaumuhimu sana kwetu sisi wakazi wa mdmni inatusaidia sana kwanza kuzuia upepo mkali unaotoka baharini pia inatusaidia uwepo wa mazalia ya samaki kwani sisi shughuli yetu kuu ni ufugaji na uchokoaji.”anasema.

Anasema kipindi mikoko ilivyoanza kuanguka na mingine kukauka maji ya baharini yalianza kusogea taratibu katika maeneo yao hali iliwafanya kujawa na hofu ya maeneo kuchukuliwa na maji.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mdimni,Adamu Ulanga anaelezea namna hatua walizochukua katika kuhakikisha wanakabiliana na athari zilizojitokeza katika upoteaji wa misitu ya mikoko hekari 1000.

Anasema wanakijiji kwa kushirikiana na uongozi wa kijiji ulianza kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha wanarudisha uoto huo wa asili kwa kuhakikisha wanaunganisha nguvu za pamoja.

Ulanga anasema awali ya yote wanakijiji walikutana na wataalam mbalimbali wa mazingira na kuelezwa sababu ya kijiji chao kuathirika na mabadiliko ya tabianchi baada ya mvua kubwa ya ndani ya miaka miwili kunyesha.

Anasema waligundua kuwa chanzo cha mikoko hiyo kuathirika na kukauka zaidi ya hekari 1000 na kuathiri fukwe ni pamoja na maji ya baridi kuzidi katika fukwe za mto na kusababisha misitu hiyo ya mikoko kutoweka.

“Baada ya kugundua hayo,tuliamua kwa umoja wetu kuanza harakati ya kurejesha miti iliyoharibika na kupotea kwa kuanza kupanda  miti zaidi ya Milioni moja ambapo miti hiyo ilikuja kufa baada ya kutofata utaalamu wa upandaji wa mikoko katika eneo hilo,” anasema.

“Baada ya kuona hali hiyo inajirudia mara kwa mara ndipo tuliamua kutafuta wataalamu wa mazingira kutoka taasisi mbalimbali walitusaidia kutufundisha juu ya upandaji wa miti hiyo kwa ustadi ambapo hadi sasa imekuwa na kustawi vizuri.”

Anasema baada ya miti hiyo kuanza kukua pia kijiji sasa kimeamua kuanzisha vitalu (nursery) vya miti ya mikoko itakayosaidia kukuza upandaji wa miti hata maeneo mengine ambayo yapo hatarini kuathirika na mabadiliko ya tabianchi.

Ulanga anasema uanzishaji wa nursery hiyo ya mikoko imetokana na hali ya wao kuwa wahanga wa utafutaji wa mikoko pindi walipokuwa wakirudha uoto huo wa athiri.

Anasema katika nursery hizo walizozianzisha ambazo tayari wameanza kupanda mbegu hizo hadi kufikia Juni mwaka huu wanatarajia kuzalisha vitalu zisivyopungua 50,000.

“Mbali na hayo sisi pamoja na serikali ya kijiji na Vikundi vya utunzaji wa mazingira (BMUW )tuliamua kuunda vikundi katika kijiji chetu cha ufugaji wa nyuki ikiwa ni mikakati ya kuhakikisha misitu hiyo inatunzwa na kuangaliwa kwa ukaribu wa hali ya juu  ili kupunguza kasi ya uharibifu na kuwa walinzi wa msitu wetu wa mikoko,” anasema.

“Tuna mwaka mmoja tangu kuanza kupanda miti hii, awali tulikuwa tunapanda miti kwa kujazia tu ili eneo lisiendelee kulika na hatukuwa na utaalamu wowote, ila tuliposhirikiana na wataalam mawazo yaliongezeka na kuanza kupanda kwa kitaalamu”anasema.

Anasema kupitia vikundi hivyo walikubaliana kila mwanakikundi mmoja kuhakikisha anapanda mti mmoja kwa siku ambapo kwa mwaka kila mmoja anatakiwa kupanda miti 360 ambapo kwa mwaka 2023 wanamiti 616,000 wanayoirekodi na kuifanyia tathimini.

***MAMLAKA YA MISITU INAZUNGUMZIAJE

Mhifadhi Misitu wa TFS, Wilaya ya Mkuranga, Charles Kaselya anasema baada ya eneo hilo kuharibika na mabadiliko ya tabianchi,TFS iliweza kuchukua hatua mbalimbali za kukabilikana nayo huku ikishirikiana na wananchi wanaoishi katika eneo hilo.

Anasema miongoni mwa hatua walizochukua ni pamoja na kuanza kurejesha miche ya mikoko kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kimazingira ambapo waliweza kurudisha uoto wa asili katika ukanda huo kwa kupanda miche ya mikoko tena.

“Mbali na hiyo tumeweza kuungana na wananchi wa eneo la mdmni na kuwapa  elimu ya utunzaji wa misitu hiyo ya mikoko kwa kuwaanzishia fursa mbalimbali ikiwemo ya  ufugaji wa nyuki  na uhifadhi wenyewe wa misitu ili kuhakikisha mikoko hiyo inalindwa na kutunzwa kwa umakini,” anasema.

“Tumeweza kuhamasisha ufugaji wa samaki katika eneo hilo na kutenga eneo kwaajili ya wananchi kuweza kulima mchicha kwa kufanya hivi tumeamua kuhusisha shughuli za kibinadamu katika maeneo haya ili kuweza kulinda vyanzo hivyo.” anasema.

Akisimulia sababu ya uwepo wa tatizo hilo kitaalamu ambalo lilianza kati ya 2019 hadi 2020, Kaselya anasema mvua kubwa ilionyesha na kuathiri eneo hilo la mikoko ni kutokana na  maji baridi ya bahari kuwa mengi zaidi na kuzidi maji ya mchanganyiko ya joto.

Anasema maji hayo yaliyozidi kiwango kikubwa ya ubaridi yaliingia katika maeneo ya fukwe na kufanya uharibifu ambapo miti ilianza kukauka na mingine kuanguka kutokana na kupoteza hali ya uhimili wa kuishi katika ardhi.

Kuhusu sheria ya Utunzaji wa Misitu ya Mikoko,  mhifadhi huyo anasema ipo katika sehemu mbili ya uhifadhi na ya wananchi. ‘’Sheria inasema hairuhusiwi kufanya shughuli za kukata miti,kujenga pembezoni mwa uhifadhi wa msitu wa mikoko,kulima ,kuweka kambi  na kufanya shughuli nyingine haziruhusiwi,’’anasema.

Anasema Sheria za misitu namba 14 ya mwaka 2002 kifungu namba 26(a)na (b)imekataza mtu yoyote kufanya shughuli za hifadhi katika maeneo ya misitu ya mikoko.

Kaselya anasema katika kutekeleza hilo wamekuwa wakifanya doria mbalimbali za kukagua maeneo hayo ambapo kwa mkuranga eneo lenye misitu ya mikoko ipo takribani 3,489 na endapo  mtu atakaekutwa anafanya makosa hayo anakamatwa na kupelekwa mahakamani.

Akizungumzia bajeti ya upandaji miti ya mikoko katika kurudishia maeneo yaliyoathirika,anasema Serikali inatoa kiasi cha sh. Milioni 5 kila mwaka katika kuhakikisha kunafanyika zoezi la urudishiaji wa mikoko iliyoathirika katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri.

***HALI ILIVYO MDIMNI

Kaselya anasema kwa sasa  uoto wa misitu ya mikoko katika eneo hilo upo vizuri,kama kipaumbele cha nchi kinavyohimisza juu ya utunzaji wa mazingira ni misitu kwanza.

Anasema kijiji cha Mdimni ni moja ya eneo ambalo lenye msitu wa mikoko bora kuliko maeneo yote ya Wilaya ya Mkuranga ambapo eneo lote la mikoko linaukubwa wa zaidi ya 1000 na eneo lililoharibika lilikuwa  hekari 64.

Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Andrew Komba anasema mikoko ni jamii ya misitu hivyo Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira imekuwa ikiandaa sera na miongozo mbalimbali kwa Wizara na taasisi  zinazosimamia masuala ya mazingira.

Anasema katika miongozo hiyo na sera  hizo wanazoziandaa zinakuwa zikihamasisha Taasisi husika na Wizara mbalimbali kama yaMaliasili na Utalii kuhakikisha inafata miongozo hiyo na kuelekeza wananchi kuchukua hatua ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi huku serikali ikitoa fedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko hayo.

Anasema wao wamekuwa wakishuka katika Wizara na taasisi hizo kuhakikisha wanafata sera na kuhamasisha wananchi juu ya utunzaji wa mazingira na kuchukua hatua endapo mabadiliko ya tabianchi yanapotokea.

“Tunataka Mikoko isikatwe ndio maana tunatoa Miongozo,Masterplan kuzungumzia uharibifu wa Mikoko na madhara yake na endapo isipotunzwa vizuri inaweza kuleta madhara  hivyo tumekuwa tunawaambia watu wasekta husika kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi na kuhakikisha wanawapa wananchi shughuli mbadala ili kuhakikisha hawafanyi uharibifu wowote kama ukataji wa miti ovyo,’’anasema.