February 27, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanahabari wataka magari maalum misafara ya viongozi

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

UONGOZI wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya,umeisisitiza Serikali kuweka magari maalum kwa ajili ya waandishi,pindi wanapokua kwenye misafara ya viongozi ili kuepuka ajali ambazo zimekuwa zikisababisha ulemavu wa kudumu pamoja na vifo.

Hii ni baada ya ajali iliotokea Februari 25,2025 majira ya jioni,eneo la Shamwengo Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, ikihusisha gari la Serikali aina ya Land Cruiser mali ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mbeya iliyokuwa imewabeba Waandishi wa Habari wanne na baadhi ya maofisa wa Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Februari 26,2025,Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya,Nebart Msokwa,amesema ajali hiyo iliyoua watu watatu akiwemo Mwandishi Habari wa kujitegemea ,Furaha Simchimba, ambao walikuwa wakitokea Wilaya ya Mbarali kwenye ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa,Fadhili Maganya.

“Tunapokuwa kwenye misafara ya viongozi iandaliwe gari maalum kwa ajili ya Waandishi wa Habari,ili tuweze kufanya kazi zetu za kitaaluma lakini pia tusikimbizane na misafara bila sababu huku tukitumia magari ambayo hayana uwezo wa kukimbizana,”amesema Msokwa.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo amesema, kulingana na uzoefu waliopata wakati wa ziara ya kiongozi wa siku ya kwanza waliachwa Mbeya Vijijini wakiwa hawana gari na kulazimika kuomba kukaa kwenye gari la Mbunge wa Mbeya Vijijini ambalo nalo lilikuwa limejaa na kulazimika kuomba kukaa nyuma.

“Licha ya kujibana kwenye gari hilo nyuma bado walipigwa na vumbi ambayo ni hatari kwa maisha yao,baada ya kulalamika siku iliyofuatwa walipatiwa gari aina ya Land Cruiser ambayo bado hawakuwa huruma nayo kutokana na kuchanganya na baadhi ya Maofisa wa CCM,”amesema.

Amesema kuwa gari hiyo iligongana uso kwa uso na basi la kampuni ya CRN, ambayo ilikuwa ikitokea mkoani Mbeya kuelekea wilayani Mbarali.

Aidha Msokwa amewataja waandishi wa habari watatu waliojeruhiwa kuwa ni Epimacus Apolinary kutoka Channel Ten ambaye amejeruhiwa mguu eneo la paja na meno kutoka,Seleman Ndelage kutoka Dreem FM ambaye alivunjika mguu na kupata majeraha mgongoni na taya huku Denis George alivunjika mkono na kupata majeraha sehemu za kichwani.

“Wenzenu hawa baada ya kupata ajali walikimbizwa katika hospitali ya Wilaya ya Inyala kwa ajili matibabu na baadaye walihamishwa katika hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Mbeya,ambako wanaendelea na matibabu na mwili wa marehemu Simchimba umehifadhiwa hospitali ya wilaya ya Inyala, “amesema.

Kwa upande wake Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini,Dkt.Tulia Ackson amepata fursa ya kufika hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kuwajulia hali majeruhi ambao wanaendelea kupatiwa matibabu.