April 29, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanahabari wapewa mafunzo kuzuia ukatili wa kijinsia kazini

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Imeelezwa kuwa ukatili dhidi ya wanawake waandishi wa habari nchini,ni ishara ya unyanyapaa na unaweza kusababisha madhara mbalimbali, kama vile kuongezeka kwa msongo wa mawazo,wasiwasi,mfadhaiko,woga wa kujihusisha na mijadala muhimu ya umma,kutojiamini katika kutoa maoni.Yote haya yakichochewa na kuhofia kutendewa ukatili zaidi.

Hayo yamebainishwa Aprili 15,2025,na Mkuu wa Mawasiliano na Habari,waTume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Christina Musaroche,kwa Niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Profesa Hamisi Malebo,wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari mkoani Mwanza,juu ya ukatili dhidi ya waandishi wa habari wanawake.

Christina,amesema unyanyasaji wa wanawake waandishi wa habari iwe kwenye vyombo vya habari au nje,unasababisha kukosekana kwa ari ya kupenda kazi na madhara mengine ambayo yanaweza kuathiri ubora wa kazi zinazofanywa na wanawake waandishi wa habari.

Amesema kwa kuzingatia changamoto hizo,Tume hiyo imeona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo ili kuunga mkono juhudi za Serikali,katika kukabiliana na matishio mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwaathiri wanawake waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao.

“Tunaamini kupitia mafunzo haya, wanawake waandishi wa habari na wadau wote wa habari,watapata maarifa yatakayowawezesha kuboresha utendaji kazi,ili kuleta tija.Pia ni msingi muhimu katika kupambana na kukabiliana na unyanyasaji dhidi ya wanawake waandishi wa habari,unaofanywa kwa namna yoyote na mtu,kikundi au mamlaka zozote,”.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza(MPC), Edwin Soko, amesema,mafunzo kama hayo yanawatayarisha waandishi wa habari kuwa makini hasa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Siyo waandishi wa habari tu,lakini katika sehemu za kazi zote ripoti mbalimbali zinaonesha kwamba wanawake ndio wamekuwa wakiathiriwa zaidi kwenye utendaji kazi iwe za kiuandishi au sekta nyingine.

Soko amesema,kwa tafiti zilizofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania(TAMWA), unyanyasaji wanawake kwenye vyombo vya habari ni mikubwa.

“Kama ndio hivyo,lazima tuchukue njia madhubuti na kuwa na mpango kazi wa kuhakikisha tunawafundisha waandishi hawa.
Tume ya Taifa ya UNESCO kwa kushirikiana na MPC,imetoa mafunzo kwa waandishi wa habari,hivyo tunaamini wakirudi kwenye vyombo vyao watahakikisha kuwa kunakuwa na sera kwenye vyumba vya habari,madawati maalumu ambayo yatasaidia kufanya tathimini na kupunguza ukubwa wa tatizo,”.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo,Chausiku Saidi,amesema,unyanyasaji mkubwa wanaoupata waandishi wa habari wanawake ni wa kingono.

Ambao ameeleza kuwa,unasababisha kushindwa kutekeleza majukumu yao pamoja na kuounguza ujuzi katika kazi.

“Ukiangalia katika tasnia ya uandishi wa habari wanaume ni wengi kuliko wanawake kwa sababu ya vitendo hivyo.Naomba tupate pa kusemea changamoto zetu kwa kuwekwa madawati ya kijinsia ambayo watu wake watakuwa na usiri,”.