Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Wanafunzi wawili wa shule ya msingi ya mchepuo wa kiingereza Blessing Model iliyopo Nyasaka,Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza,wanadaiwa kutekwa.
Akizungumza Februari 5,2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, amesema,jeshi hilo linafuatilia tukio la kutekwa kwa watoto hao pamoja na kuwasaka watu wanaotuma jumbe fupi kwenye uongozi wa shule ya Blessing Model,wakitaka wapatiwe kiasi cha fedha ili waweze kuwaachia huru watoto hao wakiwa salama.
Mutafungwa amesema, Februari 05,2025 majira ya saa 12 na dakika 10,alfajili (06:10hrs), eneo la Capripoint,barabara ya Nassa,Wilaya ya Nyamagana, gari yenye namba za usajili T. 233 DJC,Toyota Hiace, mali ya shule ya Blessing Model,likiwa na wanafunzi 6 kati yao darasa la awali mmoja na msingi watano.Ambao tayari wazazi wao walikuwa wamemkabidhi dereva na Matron wa gari hilo kwa ajili ya kuwapeleka shuleni.
Wakiwa eneo hilo la Capripoint kabla ya kuanza safari, dereva aliamua kumsaidia usafiri kwa kumpandisha mtu mmoja wa jinsi ya kiume kwenye gari hilo aliyemuambia kuwa anaelekea mjini.
Inadaiwa mtu huyo alikaa nyuma ya kiti cha dereva wa gari hilo na umbali mfupi baada ya kuanza safari katika barabara hiyo ya Nassa ghafla abiria huyo alibadilika na kumkaba dereva shingoni na gari kusimama.
Pia ameeleza kuwa ,katika vurugu hizo abiria huyo alifanikiwa kufungua mlango wa gari na kuwabeba wanafunzi wawili,kisha kuondoka nao kwa kutumia usafiri wa pikipiki mbili ambazo namba za usajili bado hazijafahamika.
Amewataja watoto waliotekwa wametambuliwa majina yao kuwa ni Magreth Thobias Juma(8), mwanafunzi wa darasa la pili na mkazi wa mtaa wa Hesawa, Capripoint na Fortunata Geofrey Mwakalebela,(5) mwanafunzi wa darasa la kwanza na mkazi wa Bugando.
Wanafunzi wengine waliobaki ambao idadi yao ni 4, hawakupata madhara yoyote,tayari wamekabidhiwa kwa wazazi wao na viongozi wa shule.
Hata hivyo Mutafungwa amesema,uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea ili kuwakamata wahalifu hao sambamba na kuwapata watoto wakiwa salama huku Watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo ni Richard Melkioli Mtui(34) mkazi wa Nyasaka na Rebeca George Kijazi(23) mwalimu na mkazi wa Nyasaka, wilayani Ilemela.
“Chanzo cha tukio hili ni tamaa ya kupata fedha, kwani uongozi wa shule ya Blessing Model,wameanza kupokea ujumbe mfupi kupitia simu za mkononi kutoka kwa mtu anaejitambulisha kuwa anataka atumiwe fedha ili awaachie watoto hao.Ufuatiliaji wa makachero wa Jeshi la polisi unaendelea,”.
Ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano utakaowezesha kupatikana kwa watoto hao wakiwa salama pamoja na kuwatia mbaroni watuhumiwa wote.
Sanjari na hayo ametoa wito kwa wakuu wa shule zinazotumia magari kusafirisha wanafunzi kwenda na kurudi shuleni, kuweka uangalizi makini kwa watoto pia magari ya shule yasibebe abiria ambao ni tofauti na wanafunzi.
More Stories
Kamishna wa Zimamoto atoa pole kwa waathirika wa majanga ya moto
Adaiwa kumuua mpenzi wake,naye kujinyonga
EWURA yatangaza bei kikomo za mafuta