Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Lushoto
WANAFUNZI watatu kati ya saba walioingia kwenye kumi bora kitaifa kidato cha sita mwaka 2022 ambao walishika nafasi ya sita, saba na nane kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St. Mary’s Mazinde Juu, wamepata Scolarship ya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Pia, wanafunzi wanne kati ya hao akiwemo mshindi namba moja (Tanzania One) Chatherine Alphonce Mwakasege na wenzake walioshika nafasi ya pili, nne na tano, wao wamepata Scolarship ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Lakini pia shule hiyo imeendelea kuwa tishio nchini baada ya wanafunzi wake 140 kati ya 149 waliofanya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne 2022, kupata daraja la kwanza (division one) na tisa kupata daraja la pili, huku kukiwa hakuna daraja la tatu, nne wala sifuri.
Hayo yalisemwa Februari 11, 2023 na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana St. Mary’s Mazinde Juu iliyopo Magamba, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Mtawa Evetha Kilamba.
Ni kwenye mahafali ya 26 ya kidato cha sita ya shule hiyo, ambapo wanafunzi 286 walihitimu masomo ya ngazi hiyo.
“Bado tumeendelea kuaminika kwenu wazazi kwa kuwa tunaendelea kusimama vizuri kitaaluma.”
Tangu mwaka 2011, shule yetu imekuwa ikifanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha sita.
Kwa mfano mwaka 2022 wanafunzi waliomaliza walikuwa 296, ambapo daraja la kwanza walikuwa 256, daraja la pili 38, daraja la tatu mmoja, na hakukuwa na daraja la nne wala ziro.
“Katika matokeo hayo, shule ilishika nafasi ya 12 kitaifa, na nafasi ya pili kimkoa, ambapo wanafunzi saba waliingia kumi bora kitaifa. Na kati ya hao, wanne akiwemo aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa yaani Tanzania One Catherine Alphonce Mwakasege, wamepata Scolarship ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Na wengine watatu wamepata Scolarship ya Mama Samia Suluhu Hassan” alisema Kilamba.
Kilamba aliwataja wanafunzi hao saba na nafasi zao kwenye mabano, Catherine Mwakasege (mwanafunzi wa kwanza kitaifa- PCB), Lucy Magashi (nafasi ya pili kitaifa- PCB), Minael Mgonja (nafasi ya nne kitaifa- PCB), na Norah Kidjout (nafasi ya tano kitaifa- PCB), hao wanasomeshwa na BoT.
Wanaosomeshwa na Rais Dkt. Samia ni Jenipher Chuwa (nafasi ya sita kitaifa- PCB), Pauline Mabamba (nafasi ya saba kitaifa- PCM) na Rachel Moshy (nafasi ya nane kitaifa- PCM).
Pia katika kumi bora ya wasichana kitaifa ya kidato cha sita 2022, Dina Ngiga (PCB) alishika nafasi ya nane, na Lisa Assey (EGM) alishika nafasi ya sita kwenye kumi bora kitaifa katika mchepuo wa sanaa.
“Kwa kidato cha nne mwaka 2022 walikuwa wanafunzi 149, ambapo daraja la kwanza ni 140 na daraja la pili ni tisa, na hakuna daraja la tatu, nne wala sifuri.”
Kwa utaratibu mpya, hakuna upangaji uliofanyika kuonesha nafasi ya shule, ila wapo waliofanya vizuri zaidi kwa kupata daraja la kwanza ya pointi saba mpaka tisa.
Wanafunzi 39 walipata pointi saba, wanafunzi 16 wakapata pointi nane (8), na wanafunzi 15 walipata pointi tisa.”Katika mtihani huo kuna wanafunzi wetu ambao wamepata ufaulu wa juu kwa kupata alama “A” katika masomo yote, mfano mwanafunzi wetu Khadija Hassan Mmuni, yeye ni mmoja wa wanafunzi wenye “A” zote” alisema Kilamba.
Kilamba amelishukuru Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa kutambua mchango wa shule zinazosimamiwa na Kanisa Katoliki, ambapo katika utambuzi huo, Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St. Mary’s Mazinde Juu imetajwa na TEC kuwa imefanya vizuri kwa kupata Daraja A ambayo ni Excellent.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa