Na Thomas Kiani, TimesMajira Online, Singida
WANAFUNZI wawili wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Msungua, Hamisi Juma na Stumai Hassani wote wa Kijiji cha Msungua, Kata ya Sepuka, Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida wameng’atwa na pakapori mwishoni mwa wiki iliyopita wakiwa darasani katika shule hiyo wakati wakiendelea na masomo.
Habari zaidi juu ya tukio hilo zinasema pakapori huyo anayedhaniwa kuwa na ugonjwa wa kichaa alionekana kwa mara ya kwanza chooni kwa mganga kiongozi wa zahanati ya kanisa lililopo kwenye kijiji hicho saa 4:00 asubuhi Agosti 13, mwaka huu, wakati alipokwenda kupata huduma.
Mganga Kiongozi wa zahanati hiyo Dkt.Baraka Sombi amesema alimkuta pakapori huyo chooni na alipompiga teke akaking’ata kiatu akampiga tena teke kwa mguu mwingine akakimbia.
Dkt.Sombi amesema alipoona hali hiyo akaenda kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kitongoji Msungua kati,Issa Jingi ambapo alikutana na wanakijiji akaelezwa kuwa pakapori huyo amewang’ata wanafunzi wawili shuleni na wamepelekwa Kituo cha Afya Sepuka kutibiwa.
Hata hivyo mwalimu Mkuu wa shule Julius Lema amesema yeye hana habari zozote kuhusu tukio hilo la wanafunzi wake kung’atwa na pakapori kwa sababu walimu wa zamu Athumani Bakari hajampa taarifa hizo na mwalimu wa darasa hilo Juma Omari hajampa taarifa hata hivyo wanafunzi waliong’atwa na pakapori huyo walipelekwa Kituo cha Afya Sepuka na mmoja kati ya walimu wake akitumia pikipiki yake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi, Stumain Hassani, amesema aling’atwa na pakapori huyo kwenye mguu chini ya goti na alimweleza baba yake mlezi Hamis na alipelekwa kituo cha afya Sepuka na mwalimu Salehe Mtinda na pikipiki yake.
Baada ya wanafunzi hao kufikishwa kituoni walipata chanjo ya TT na kuambiwa na mganga warudi tena kuendelea na chanjo hiyo tarehe Septemba 13, mwaka huu,pia amewaambia waende mkoani Singida kupata chupa tano za kutibu ugonjwa wa kichaa cha mbwa.
Wakidhibitisha kuhusiana na tukio hilo wazazi wa Hamis Juma wamesema mtoto wao alipofika nyumbani aliwaeleza kuwa aling’atwa na pakapori mguuni na akapelekwa kituo cha afya Sepuka kutibiwa, ameambiwa arudi tena kupata chanjo ya TT na pia zinahitajika chupa tano za kutibu ugonjwa na zitatunzwa kituoni.
Aidha kwa mujibu wa wanafunzi wamesema kuwa baada ya pakapori huyo kuwang’ata wanafunzi hao alikimbia nje akakimbizwa na walimu huku wakiwa na wameshika fimbo na miti walianza kumpiga hadi kufa.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE), linasema watu 55,000 hupoteza maisha kila mwaka kwa kupata kichaa cha mbwa kwa kukosa matibabu sahihi au kutokufahamu ugonjwa wenyewe vyanzo vyake na mnyama anapopata ugonjwa huo hachagui mazingira.
Shirika hilo limesema dalili za sehemu zilizopata majeraha hufa ganzi na virusi vikishaanza kuchanganyika na damu huleta madhara kwa muhusika hivyo ni muhimu sana inapotokea tukio hilo ni vyema wanganga wakasimamia vizuri kutibu ugonjwa huo kikamilifu.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani