November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi wa Diploma kozi za kimkakati NIT sasa kupata mikopo

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online

CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimewaasa vijana waliohitimu kidato cha nne kuchangamkia fursa ya kuomba kusoma kozi zakimkakati katika mwaka wa masomo wa 2024/2025 ili wanufaike na fursa ya kupata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kuanzia ngazi ya diploma.

Hayo yamesemwa na Afisa Uhusiano wa Chuo hicho Juma Manday wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara jijini Dar Es Salaam ,banda la NIT huku akisema kozi hizo zimepata upendeleo wa mkopo kuanzia ngazi ya diploma ili kupata wataalam wengi watakaoshiriki katika ujenzi wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa hivi sasa na serikali ya awamu ya sita.

Amesema kozi hizo zimepewa kipaumbele na serikali ya awamu ya sita kwa sababu ni muhimu kwa ajili ya miradi ya kimkakati.

“Kwa sasa tuna kozi nne za kipaumbele ambapo waombaji kuanzia ngazi diploma watapata mkopo kama wanavyopata wale wa shahada ya kwanza,tunaishukuru serikali yetu ya awamu ya sita kwa kutoa huu msukumo kwa ajili ya kuwezesha kupata wataalam watakaofanya kazi katika miradi ya kimkakati inayotekelezwa hapa nchini.”amesema Manday

Amesema kozi hizo ni kwa ajili ya kuandaa wataalam mbalimbali ikiwemo mafundi na wahandisi wa kutengeneza ndege,wataalam wa kujenga na kukarabati meli,wataalam wa mafuta na gesi na wataalam wa kusimamia shughuli za bandari kwa maana ya kukuza uchumi wa Buluu.

“Ipo miradi mikubwa kama mradi wa kufufua Shirika la Ndege la Air Tanzania,mradi wa kujenga viwanja vya ndege na kuvipanua,haya yote yanahitaji wataalam ambao sasa watatoka katika Chuo chetu cha NIT.”amesema Manday

Aidha amesema kutokana na wataalam hao kuwa wachache ,serikali ya awamu ya sita imeona kuna umuhimu wa hizi kozi kupata upendeleo kwa ajili ya kutoa msukumo kwa watanzania wengi kusoma kwa ajili ya kupata wataalam wazawa.

Akitolea mfano wa wahandisi wa kujenga na kukarabati meli wapo nchini lakini ni wachache ,wakati nchi inaitekeleza mradi wa kujenga meli mpya na kuzifanyia ukarabati meli za zamani.

Amesema upatikanaji wa wataalam hawa hapa nchini utasaidia kuokoa fedha nyingi ambazo hutumika kuchukua wataalam kutoka nje ya nchi.

Manday ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa vijana waliohitimu kidato cha nne na wenye sifa stahiki kuchangamkia fursa kuomba kusoma kozi hizo kwani dirisha la udahili kwa ngazi ya cheti na diploma limeshafunguliwa.