November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi takriban 1500 wapewa wiki mbili kuripoti shuleni



Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Mwanza

Takribani wanafunzi 1500 sawa na asilimia 10 wa kidato cha kwanza bado hawajaripoti shule katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela hadi Februari 1,2023.

Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Massala,ametoa wiki mbili kwa viongozi kuhakikisha wanafunzi hao wanaripoti shuleni ili kufikia asilimia 100 ya wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao wameripoti shule.

Massala ametoa agizo hilo katika kikao kazi cha kufanya tathmini ya ufuatiliaji wa uandikishaji wa darasa la awali, la kwanza na hali ya kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023 katika shule za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

Kilichowakutanisha Watendaji wa Kata na Mitaa,Ofisa Elimu Kata,Wakuu wa shule za sekondari, Wenyeviti wa Bodi za shule pamoja na Wenyeviti wa mitaa, kilichofanyika wilayani Ilemela.

Massala ameeleza,watoto 1500, ni wengi wakiwaacha wapotelee huko mtaani kama Wilaya,Mkoa na taifa watapata hasara na kikatiba ni haki yake mtoto kupata elimu hivyo amesisitiza kuhakikisha wanafunzi hao wanaripoti ndani ya muda huo.

Mbali na changamoto nyingine ukosefu wa utambuzi kwa wazazi juu ya kuwekeza katika elimu ya watoto wao imechangia .

“Tukiondoa wale ambao wamepelekwa shule binafsi,hao watoto wapo nyumbani,tumefuatilia kupitia watendaji wetu, kwenye baadhi ya maeneo,Wakuu wa shule andaeni majina ya watoto wote waliochaguliwa katika shule zenu muwakabidhi watendaji na Wenyeviti wa mitaa ni wajibu wetu kuhakikisha watoto walio salia wanaripoti shuleni,”ameeleza Massala.

Huku akihimiza shule ambazo zina idadi kubwa za wanafunzi ambao hawajaripoti kuhakikisha wanaripoti kwa haraka ikiwemo Shibula ambayo ilipangiwa wanafunzi wa kidato cha kwanza 647 ambapo mpaka sasa wanafunzi 212 bado hawajaripoti shule ambapo ametoa wiki moja kwa viongozi wa Kata ya Shibula kuhakikisha watoto hao wanaripoti shule.

Hivyo amemtaka Mwalimu kiongozi wa Shibula,kutoa idadi ya wanafunzi kwa majina waliopangwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule hiyo kisha amkabidhi Ofisa Mtendaji wa Kata ambaye atakaa na watendaji wake kuona namna gani watawapata watoto hao kwani ametoa wiki moja ya kuhakikisha wanafunzi hao wanaripoti shuleni.

“Tuwatafute hao watoto nawapa wiki moja kuanzia tarehe ya leo Februari ,2,2023,wiki ijayo tupokee ripoti ya Kata kwa Kata tukianzia Kata ya Shibula,mpango ni wenu mtatumia njia gani ili muwapate hao watoto,nyumba kwa nyumba,mlango kwa mlango,kitanda kwa kitanda shuka kwa shuka mpaka hao watoto waingie madarasa,”.

Mbali na Shibula ameeleza kuwa shule ya Kiloleli ambayo imepangiwa wanafunzi 386 na walioripoti ni 268 huku ambao hawajaripoti ni wanafunzi 118 sawa na asilimia 31, Buzuruga ilipangiwa watoto 730, walioripoti ni 583 huku watoto 147 hawajaripoti,Ofisa Elimu utawapa hizi takwimu ili kila Kata ione ipo katika nafasi gani.

Sanjari na hayo Massala ameeleza kuwa kwa upande wa elimu msingi hadi kufikia Februari 1 mwaka huu jumla ya wanafunzi 7706 wa darasa la awali sawa na asilimia 103 na wanafunzi 11,221 wa darasa la kwanza sawa na asilimia 106 wameandikishwa na kuripoti shule.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Masemele Kata ya Shibula Yohana Sukari, ameeleza kuwa umbali wa shule ya sekondari unaweza kuwa sababu ya wanafunzi waliopo katika Kata hiyo wa kidato cha kwanza kushindwa kuripoti shuleni.

“Unakuta mtoto anatembea umbali mrefu takribani kilomita 15, na anaenda kwa miguu na wengine wanatumia baiskeli na barabarani kuna shida kuna sehemu kuna michanga mingi,mashimo lakini tunampango wa kujenga shule ya sekondari kwenye maeneo yetu ya karibu.

Sukari ameeleza kuwa Kata yao ipo kando ya Ziwa,kuna baadhi ya wazazi ambao wamekuja kwa ajili ya shughuli za uvuvi na wana hama hama,hivyo ikitokea mwanafunzi kabebeshwa mimba familia inahama kwenda kisiwani na hao pengine ndio wanaochangia idadi ya wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni kuwa kubwa.

“Kufuatia agizo la Mkuu wa Wilaya,tutapita shuleni tujue nani amefaulu na amepangiwa kwenda wapi na tufuatilie kule alikopangiwa kama ameripoti na wazazi watuambie watoto wao wapo wapi, kama ameenda shule nyingine tunafuatilia kuwa yupo shuleni kweli na je ameisha ripoti na anaendelea na masomo ili tupeleke taarifa kwa Mkuu wa Wilaya,”ameeleza Sukari.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Semba’B’ Kata ya Shibula Grace Leopard, ameeleza kuwa changamoto ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kutoripoti ni kutokana na mazingira yao ya kuishi mwambao mwa Ziwa Victoria kunakofanyika zaidi shughuli za uvuvi.

Kwani wazazi wengi hawana muamko wa kupeleka watoto shule badala yake wanawaacha waende kufanya shughuli za uvuvi.

“Tunajitahidi kuwaelimisha wazazi lakini wanaona mtoto akienda shule anachelewa katika shughuli za uvuvi, serikali ituunge mkono kuelimisha wazazi juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto ambayo ndio msingi kuwa itamfanya afanye kazi vizuri ata kama ni ya uvuvi,”.

Ameeleza kuwa katika kutekeleza agizo la Mkuu wa Wilaya atafanya kikao na wananchi kwa ajili ya kuwaelimisha umuhi elimu hivyo wawaache watoto waende shule.

“Hata mimba za utotoni zinatokana na mtoto wa kike kutojielewa kwani wakienda ziwani lazima washawishike na pesa za wavuvi pia nitatembelea shuleni kuwaeleza wanafunzi kuwa elimu ndio msingi wa maisha,”ameeleza Grace.