Na Suleiman Abeid, TimesMajira Onloine, Shinyanga
WANAFUNZI wa Chuo cha Uuguzi cha Kolandoto Manispaa ya Shinyanga wameshauriwa kuzingatia michezo ili kuweza kuboresha afya zao na pia waelewe michezo inaweza kuwapatia ajira.
Ushauri huo umetolewa na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kolandoto (WEO), Jacob Mwakaluba aliyekuwa mgeni rasmi katika Bonanza la michezo ambalo limeandaliwa na Wanachuo cha Uuguzi cha Kolandoto likienda sambamba na upandaji wa miti kwa lengo la kutunza mazingira katika maeneo ya Chuo.
Mwakaluba amesema, michezo ni muhimu kwa kila mtu kwa vile mbali ya kuimarisha afya lakini inachangia kuimarisha udugu miongoni mwa jamii na huweza kuwapatia ajira nzuri hapa nchini na hata nchi za nje mfano ilivyotokea kwa baadhi watanzania wanaocheza mpira wa kulipwa kimataifa.
“Binafsi nakupongezeni kwa kubuni utaratibu huu wa kuwa na mabonanza ya michezo hapa Chuoni, ni utaratibu mzuri na unasaidia kuwajengea afya, na lazima muelewe kuwa mbali ya michezo kuwa ni afya lakini pia ni ajira,”.
“Wapo baadhi yenu wanaona michezo kama karaha, hawa hawaoni mbali, michezo siyo karaha bali ni raha, hivyo washaurini na wahimizwe kushiriki michezo kama mnavyofanya ninyi, binafsi kwa upande wetu Serikali ninawaahidi kuwapatia msaada wowote mtakaouhitaji kutoka kwetu,” amesema Mwakaluba.
Lakini pia aliahidi kuwasaidia jezi timu ya kikapu ya chuo hicho ili waweze kushiriki bonanza la michezo la Manispaa ya Shinyanga ambalo linatarajiwa kufanyika Septemba 23, mwaka huu.
Pia amewataka wanamichezo hao hususan timu ya Kikapu kuendelea kufanya juhudi ili wafike mbali na kuwa wachezaji wakubwa ndani na nje ya nchi.
Awali katika risala yao kwa mgeni rasmi wanachuo hao wamesema, lengo la kuanzisha mabonanza ya michezo ni kutaka kuimarisha afya zao na kujenga mahusiano mazuri miongoni mwao na kupitia mazoezi wanayofanya yanasaidia miili yao kukaa vizuri na hivyo kuweza kufuatialia vyema masomo darasani.
Bonanza hilo la michezo limekwenda sambamba na upandaji miti ambapo Ofisa Mazingira, Ezra Manjerenga ambaye amewataka wanachuo sambamba na kuzingatia suala la michezo lakini pia wakumbuke umuhimu wa kupanda miti katika maeneo yanayozunguka Chuo chao ikiwemo eneo la viwanja vya michezo.
“Lengo letu Manispaa ya Shinyanga ni kuhakikisha tunapanda miti ipatayo 1,500,000 ikiwa ni lengo tulilopangiwa kitaifa, hii ni katika maeneo yote ya manispaa yetu ikiwemo maeneo haya ya viwanja vya michezo ili kuwezesha wapenzi wa michezo kuangilia michezo mbalimbali wakiwa wamekaa kwenye vivuli vya miti,” amesema Manjerenga.
Mgeni rasmi katika bonanza hilo alikabidhi zawadi mbalimbali kwa wanamichezo walioibuka na ushindi ambapo timu ya Dreamers ilikabidhiwa Kombe baada ya kuwashinda wapinzani wao kwa vikapu 39 dhidi ya vikapu 37.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025