January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi Handeni wapewa zawadi na World Vision

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Handeni

SHIRIKA la World Vision Tanzania, kupitia Mkumburu AP iliyopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, limetoa zawadi mbalimbali ikiwemo mabegi na viatu kwa wanafunzi tisa wa shule za msingi katika Tarafa ya Mkumburu, waliofanya vizuri kwenye Insha iliyoandaliwa na shirika hilo nchi nzima.

Akizungumza Juni 25, 2022 kwenye hafla fupi iliyofanyika Shule ya Msingi Michungwani ya kukabidhi zawadi hizo kwa wanafunzi tisa kutoka kata tatu za Segera, Kwedizinga na Kwamgwe, Msimamizi wa Mradi wa Elimu Mkimburu AP, Steward Mwilenga alisema nia ya shirika kuweka shindano ni katika kusaidiana na Serikali kukuza elimu, uelewa, vipaji na kupinga vitendo vya udhalilishaji kwa wanafunzi.

“Shirika la World Vision Tanzania limeandaa Insha kwa wanafunzi wa shule za msingi. Nia ya shirika ni kuhakikisha linatoa mchango wake katika kushirikiana na Serikali kuona wanafunzi wetu wanafanya vizuri kwenye masomo, huku wakionesha uwezo wao wa mtu mmoja mmoja, na vipaji katika kujua mambo.

“Mashindano haya yanakwenda sambamba na utoaji wa zawadi. Na hata leo tunatoa zawadi kwa wanafunzi tisa waliofanya vizuri kwenye shule za msingi, ambapo kwenye kata tatu za Segera, Kwamgwe na Kwedizinga tumepata washindi wa kwanza mpaka wa tatu katika kila kata, ambapo washindi wa kwanza kila kata, kila mmoja atapata zawadi ya begi moja na viatu jozi moja, huku washindi wa pili na tatu watapata kila mmoja begi moja” alisema Mwilenga.

Mwilenga alisema katika Tarafa ya Mkumburu jumla ya shule za msingi 16 zilishiriki katika mashindano hayo, ambapo jumla ya watoto 1,761 walishiriki, na kati yao, wasichana walikuwa 942 na wavulana 819 kutoka kata za Segera, Kwamgwe na Kwedizinga, ambapo kila shule ilitoa wanafunzi 10 kwa usawa wa jinsia kushiriki ngazi ya kata.

Mwilenga alisema washindi watatu wa kwanza kwenye kila kata, ni Ashura Mustafa kutoka Shule ya Msingi Kwalaguru, Kata ya Kwedizinga ambapo aliongoza wenzake kwa kupata alama 46 kati ya 50 zinazohitajika, mshindi wa pili ni Salma Kisase kutoka Shule ya Msingi Michungwani, Kata ya Segera ambaye alipata alama 45, na wa tatu ni Zuwena Simoni kutoka Shule ya Msingi Muungano, Kata ya Kwamgwe aliyepata alama 40.

Kaimu Meneja wa Mradi wa Mkumburu AP Modest Kessy alisema lengo kuu la uandishi wa Insha ni kuwezesha watoto kuweza kutoa maoni yao ya namna ya kupunguza na kutokomeza ndoa na mimba za utotoni.

“Uandishi wa Insha pia una malengo madogo madogo, yaani malengo mahususi ambayo ni kujenga uelewa kwa watoto na jamii kuhusu mimba na ndoa za utotoni na madhara yake, kukuza ujuzi wa kuandika kwa wanafunzi wa shule za msingi.

“Kuwajengea watoto hali ya kujiamini katika kutoa maoni yao kwa maandishi na kusoma mbele za watu wengi, kujua uelewa wa watoto juu ya ndoa na mimba za utotoni, na kushawishi mabadiliko ya Sera, Bajeti na Sheria zinazomlinda mtoto dhidi ya mimba na ndoa za utotoni” alisema Kessy.

Mashindano hayo ya Insha yataendelea kutoa washindi hadi ngazi ya Taifa. Baada ya mashindano hayo kumalizika ngazi ya tarafa, sasa yatakwenda ngazi ya wilaya, mkoa na Taifa.

Diwani wa Viti Maalumu wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Habiba Kizebele (kushoto) akitoa zawadi ya begi na viatu kwa Ashura Mustafa (kulia) kutoka Shule ya Msingi Kwalaguru, Kata ya Kwedizinga ambapo aliongoza wenzake kwa kupata alama 46 kati ya 50 zinazohitajika kwenye mashindano ya Insha Tarafa ya Mkumburu. Mashindano hayo yameratibiwa na kufadhiliwa na Shirika la World Vision, Mkumburu AP. (Picha na Yusuph Mussa).
Diwani wa Viti Maalumu wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Habiba Kizebele (kushoto) akitoa zawadi ya begi na viatu kwa Salma Kisase kutoka Shule ya Msingi Michungwani, Kata ya Segera ambaye alipata alama 45 kati ya 50 zinazohitajika kwenye mashindano ya Insha Tarafa ya Mkumburu. Mashindano hayo yameratibiwa na kufadhiliwa na Shirika la World Vision, Mkumburu AP. (Picha na Yusuph Mussa).
Diwani wa Viti Maalumu wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Habiba Kizebele (kushoto) akitoa zawadi ya begi na viatu kwa Zuwena Simoni (kulia) kutoka Shule ya Msingi Muungano, Kata ya Kwamgwe aliyepata alama 40 kati ya 50 zinazohitajika kwenye mashindano ya Insha Tarafa ya Mkumburu. Mashindano hayo yameratibiwa na kufadhiliwa na Shirika la World Vision, Mkumburu AP. (Picha na Yusuph Mussa).
Diwani wa Viti Maalumu wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Habiba Kizebele (wa tatu kulia) na Steward Mwilenga (wa sita kulia) ambaye ni Msimamizi wa Miradi ya Elimu Mkumburu AP, wakiwa na wanafunzi tisa, huku wakiwa na zawadi zao za mabegi, baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya Insha Tarafa ya Mkumburu, kwenye hafla fupi iliyofanyika Shule ya Msingi Michungwani. Mashindano hayo yameratibiwa na kufadhiliwa na Shirika la World Vision, Mkumburu AP. (Picha na Yusuph Mussa).
Kaimu Meneja Mradi wa Mkumburu AP Modest Kessy (kulia) akizungumza kwenye hafla fupi ya kuwapa zawadi wanafunzi tisa wa shule ya msingi waliofanya vizuri katika mashindano ya Insha Tarafa ya Mkumburu. Hafla hiyo ilifanyika Shule ya Msingi Michungwani. Mashindano hayo yameratibiwa na kufadhiliwa na Shirika la World Vision, Mkumburu AP. (Picha na Yusuph Mussa).
Watoto wa Kijiji cha Michungwani, Kata ya Segera wakiwa kwenye hafla fupi ya wanafunzi tisa wa shule ya msingi waliopata zawadi za mabegi na viatu, baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya Insha Tarafa ya Mkumburu, kwenye hafla fupi iliyofanyika Shule ya Msingi Michungwani. Mashindano hayo yameratibiwa na kufadhiliwa na Shirika la World Vision, Mkumburu AP. (Picha na Yusuph Mussa).
Wanafunzi tisa wa shule ya msingi kutoka shule mbalimbali (waliokaa) huku wakiwa na zawadi zao za mabegi na viatu, wakiwa kwenye picha ya pamoja na wazazi wao, na baadhi ya viongozi wa Mkumburu AP. Ni baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya Insha Tarafa ya Mkumburu, kwenye hafla fupi iliyofanyika Shule ya Msingi Michungwani. Mashindano hayo yameratibiwa na kufadhiliwa na Shirika la World Vision, Mkumburu AP. (Picha na Yusuph Mussa).