January 29, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi 170 wapata ufadhili wa masomo

Ashura Jumapili TimesMajira Online Bukoba

Jumla ya wanafunzi 170 waliojiunga na chuo cha King Rumanyika kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, wamepatiwa ufadhili wa masomo wa kulipiwa asilimia 50 ya ad.

Ufadhili huo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan katika nyanja ya elimu.

Hayo yamebainishwa Januari 25,2025 na Mkurugenzi wa chuo cha King Rumanyika ambaye ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba na Diwani wa Kata ya Nshambya Godsn Gypson, katika mahafali ya saba ya chuo hicho.

Gypson amesema,chuo hicho kitaendelea kutoa ufadhili ambapo wanafunzi wengine wanaoendelea kujiunga chuoni hapo watalipa asilimia 50 na asilimia 50, watalipiwa na chuo.Ambao watalipa kiasi cha 446,000 kwa mwaka badala ya 860,000.

Amesema lengo ni kushirikiana na Serikali kutoa elimu kwa jamii inayowazunguka na taifa kwa ujumla ili kumuondoa adui ujinga.

Amesema kozi zinazotolewa katika chuo hicho ni kozi ya hoteli,uhazili,uhasibu ,maendeleo ya jamii,elimu msingi na malezi ya watoto na walimu elimu ya msingi.

Hata hivyo amesema ana mpango wa kujenga chuo kingine Mkoa wa Kigoma ili kuendelea kuisadia Serikali kutoa elimu kwa Watanzani

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajath Fatuma Mwassa,amesema moja ya vitu ambavyo wamekuwa wakiviimba,kuvitetea na kuvipigania ni uwekezaji katika Mkoa wa Kagera.

Amesema kwa jitihada zinazofanywa na Mkurugenzi huyo,siku moja chuo cha King Rumanyika kitakuwa kikubwa na kutoa Shahada kwa wanafunzi wake na kujulikana kimataifa.

Hata hivyo amepongeza uongozi wa chuo cha King Rumanyika katika utoaji wa elimu bora na nafuu kwa wote,nakua mfano bora wa kuigwa ndani ya Mkoa na Taifa.

“Nawapongeza wazazi kutumia rasilimali zao kuwaendeleza kitaaluma vijana wetu kwani hakuna urithi bora tunaoweza kuwaachia watoto wetu zaidi ya elimu.Ninaamini ujuzi,taaluma na stadi walizopata zitasaidia kuboresha utendaji kazi wao na kuleta tija katika maeneo ya kazi na shughuli binafsi,”.

Huku akiwataka wahitimu hao elimu walioipata ikawe mkombozi na chachu ya kujiajiri,kwa kutumia maarifa waliyopata kuzifikia fursa mbalimbali zilizopo na zitakazopatikana kutatua changamoto ya ajira.

“Serikali inajali makundi yote hususani vijana na wanawake, katika mfuko wa mkopo hivyo nawashauri kutumia fursa ya mikopo hiyo ili kujikwamua kiuchumi,”amesema Hajat Mwassa.

Kutokana na uhaba wa soko la ajira,mitaala imebadilishwa ili kuongeza idadi kubwa ya wanafunzi ambao wataweza kujiajiri baada ya kuhitimu mafunzo yao.

Sanjari na hayo,Mkuu wa Mkoa wa Kagera amehaidi kutoa kiwanja kwaajili Mkurugezi huyo kujenga chuo kikubwa pamoja na shule shikizi ili kuendelea kutoa elimu kwa jamii .

Awali Mkuu wa chuo cha King Rumanyika, Innocent Mamerytus,amesema chuo hicho kilianzishwa mwaka 2011 kikiwa na fani za Veta,baadae wakasajili Fani za Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi ( Nactvet ) na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia.

Mamerytus,amesema mwaka wa masomo 2024/25,wanafunzi 301 wamesajiliwa na kudai kuwa wanafunzi 214 wanachukua Stashahada ya Ualimu awali na msingi huku 87 wanasoma kozi nyingine.

Amesema miongoni mwa malengo hayo ni pamoja na kujenga shule ya msingi ambayo itakuwa shule shikizi katika upimaji wa kazi ya ualimu pamoja na kujenga ghorofa mbili eneo la chuo.

Amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Kagera kuwasaidia kupata kiwanja Namba 289 kitalu B kilichopo eneo la Nyanga kwa ajili ya kujenga shule shikizi.Ambapo kiwanja hicho walikiomba kwa kumuandikia barua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba tangu Aprili mwaka 2024 hadi sasa hawajapewa majibu.

Akisoma Risala ya wahitimu Herieth Alphonce, amesema walianza masomo wakiwa wanachuo 78 lakini kutokana na majukumu na changamoto mbalimbali 10 wameshindwa kuhitimu hivyo idadi ya wahitimu ni 68.

Alphonce,anasema mafaniko yaliyopo chuoni ni pamoja na kukubalika katika maeneo yao ya kazi huku changamoto ni upungufu wa kompyuta suala linalochelewesha baadhi ya maarifa kuyapata kwa wakati.

Anasema pia kuna upungufu wa vifaa vya michezo kama vile jezi,mipira ya wavu,pete,kikapu na mpira wa miguu.