December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi wakikimbia mchakamchaka

Wanafunzi 1,600 wapatiwa mafunzo kujikinga na NCD

Mwandishi Wetu,TimesMajira,Onlibe Dar

WAKATI taifa lipo katika maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Magonjwa Yasiyoambukiza yanayofanyika kitaifa jijini Dar es Salaam, zaidi ya wanafunzi 1,600 wa shule za sekondari jijini humo wamepatiwa mafunzo ya kujikinga na kudhibiti magonjwa hayo, huku wakitakiwa kuacha mtindo wa maisha goigoi kwani ni hatari kwa maisha yao.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mafunzo hayo yaliyoanza Novemba pili, Meneja Mpango Wa Taifa wa Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Omar Ubuguye, alisema wanafunzi hasa kuanzia miaka 15 na kuendelea wapo katika hatari kubwa ya kupata magonjwa hayo wasipoepuka ugoigoi.

“Tunawapa elimu kuhusu magonjwa haya ili msiwe goigoi, lazima mfanye bidii kuepuka mtindo mbaya wa maisha unaoweza kuwaingiza katika magonjwa yasiyoambukiza, kumbukeni ninyi mpo katika hatari zaidi, ili usipatwe na magonjwa mazoezi ni lazima na mfanye bidii kula kwa kuzingatia kanuni bora, nusu ya mlo uwe mbogamboga na matunda, robo protini na robu vyakula vya wanga,” alisema Dkt. Ubuguyu na kuongeza:

“Epukeni pia matumizi ya pombe n sigara kwani yanaongoza kwa kuleta magonjwa yasiyoambukiza.”

Alisema habari mbaya sasa katika jamii ni kwamba katika kila vifo vitatu vya watu, kimoja husababishwa na magonjwa yasiyoambukiza hivyo wameamua kutoa elimu ya kujikinga na kudhibiti magonjwa hayo kuanzia shuleni, ili elimu hiyo pia iwafikie wazazi na wanafamilia wengine, lengo ni kuokoa jamii.

“Tunajenga hamsa na uelewa kwenu wanafunzi, hii iwafikie wengine, ninyi muwe viongozi kuepuka magonjwa haya. Changamoto kubwa ni nidhamu, tunapatwa na magonjwa yasiyoambukiza kwa kukosa nidhamui katika mtindo wa maisha,” alisema.

Naye Mratibu Afya na Elimu ya Afya katika shule Mkoa wa Dar es Salaam, Dokta Ndeniria Swai alisema dunia imeweka kipaumbele kwenye kupambana na magonjwa yasiyoambukiza na hata Serikali inafanya hivyo ili kuokoa watu wake.

Wanafunzi waliopewa elimu ni 346 kutoka sekondari ya Zanaki, ibasila 280, Alpha 281, sekondari ya Aboudjumbe Kigamboni wanafunzi 349 na St. Anne Maria ya Kimara kwa Msuguri wanafunzi 360.

“Tumeanza wiki ya magonjwa Yasiyoambukiza, tunatoa elimu, ninyi ndio kizazi kiinachoendeleza taifa, itumieni elimu mliyopata katikakuzuia magonjwa hayo na muelimishe wengine,” alisema Dk. Swai.

Kwa upande wake Mratibu Afya shule za msingi Wilaya ya Ubungo, Mwalimu Florence Kilasira alisema elimu kuhusu magonjwa hayo ambayo kwa yanatajwa kuua watu wengi zaidi duniani ni muhimu hasa kwa jamii ya wanafunzi kwani ndio kundi kubwa linalkotarajiwa kujenga taifa la kesho kwa kuwa ndio wazazi wa kesho na wazalishaji mali katika siku za baadaye, hivyo ni muhimu wakaishi wakiwa na afya njema.

“Maisha bila mambukizi ya magonjwa yasiyoambukiza yanawezekana, mshike mafundisho mliyopata,muwe mfano bora, nasi tutaendelea kushirikiana kuhakikisha mnapata elimu zaidi ya afya ili baadaye tuwe na taifa lisilo na magonjwa,”alisema.

Wiki ya Magonjwa Yasiyoambukiza inaanza leo kwa maandamano yatakayoianzia viwanja vya Leaders, hadi Mnazi mmoja ambapo shughuli mbalimbali zitafanyika kwa wiki nzima, ikiwamo maonyesho, upimaji magonjwa na ushauri pamoja na mkutano wa kitaaluma utakaofanyika Novemba 9 hadi 10.