December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais John Magufuli

Wanachama 2,565 wajitokeza kumdhamini Magufuli Ruangwa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Ruangwa

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameongoza wanachama 314 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Ruangwa, Lindi katika kujaza fomu za kumdhamini Rais John Magufuli ili aweze kuteuliwa kugombea tena nafasi ya urais.

Idadi hiyo inafanya jumla ya wanachama waliojitokeza kumdhamini Rais Dkt. Magufuli katika wilaya hiyo kufikia 2,565 baada ya wanachama wengine 2,251 kujaza fomu hizo jana (Jumamosi, Juni 20, 2020) na kumdhamini kiongozi huyo.

Waziri Mkuu ameongoza wanachama hao wa CCM jana leo katika ofisi za CCM wilayani Ruangwa. Amewasihi wananchi hao waendelee kuwa na imani na Rais Dkt. Magufuli pamoja na Serikali anayoiongoza.

“Rais Magufuli ametekeleza ahadi zote alizoziahidi ikiwemo ya kuwatumikia Watanzania wote hasa wanyonge. Amewatumikia Watanzania wote bila ya kujali itikadi zao za kisiasa na hata za kidini. Nawapongeza wana CCM wenzangu mliojitokeza kumdhamini rais wetu.”amesema.

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akigonganisha kiwiko na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Ruangwa, Said Kaondo baada ya kumkabidhi fomu zenye majina na saini za wana CCM waliomdhamini Rais Dkt. John Magufuli ili aweze kugombea tena urais. Tukio hilo lilifanyika kwenye Ofisi ya CCM ya wilaya ya Ruangwa, Juni 21, 2020. Katikati ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Lindi, Fadhili Juma.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa; “Kitendo mlichokifanya leo (jana) kinaonyesha shukrani kubwa kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye wakati wote ameonesha mapenzi makubwa kwetu pamoja na Watanzania wote kwa ujumla.”

Amesema kwa sasa wilaya ya Ruangwa imepata mabadiliko makubwa kimaendeleo ambayo hapo awali hayakuwepo kama nishati ya umeme, maji ambayo kwa sasa kila kijiji kina kisima, shule za msingi katika kila kijiji na sekondari kwenye kata zote pamoja na barabara za lami katika mitaa ya mji wa Ruangwa.” Haya yote ni Dkt. Mgufuli.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Lindi, Fadhili Juma amesema wanaCCM wa mkoa huo wapo bega kwa bega na Rais Dkt. Magufuli na kwamba watahakikisha anapata kura nyingi katika uchaguzi ujao.

Awali, Waziri Mkuu aliwashukuru WanaRuangwa wote kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi chote cha miaka mitano ambao ulimuwezesha kutekeleza majukumu yake ya kuwaletea maendeleo kwa ufanisi mkubwa.