Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Tabora
VIONGOZI na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Tabora,wamesema uimara wa chama hicho tangu kuanzishwa kwake,kwa asilimia 100,unachochewa na uimara wa viongozi wake kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa.
Wakiongea na gazeti hili kwa nyakati tofauti kwenye maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa CCM,wanachama wa chama hicho wamesema kuwa uimara wa viongozi wao ndio mtaji wa chama hicho kuendelea kuaminiwa na wananchi kushika dola nchini.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora,Said Nkumba, ameeleza kuwa tangu kuzaliwa Februari 5, 1977, CCM imeendelea kuthibitisha kuwa ni chama bora na chenye uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi.
Amesisitiza sifa kubwa ya chama hicho kuwa ni uimara wa Viongozi wake kuanzia ngazi ya juu hadi chini, hali ambayo inakifanya kutoyumbishwa na mtu mmoja au kikundi fulani cha watu wenye maslahi binafsi.
Sifa nyingine ambayo imekibebea chama hicho ni umoja na mshikamano wa viongozi na wanachama wake, kuanzia ngazi ya mashina hadi taifa, kuandaa makada ambao watapokea kijiti cha uongozi na kuendelea kudumisha demokrasia,
Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora,Wilson Nkambaku,amedokeza siri ya chama hicho kuendelea kuwa chaguo namba 1 la watanzania katika chaguzi zote ni uimara wa viongozi wake na uwezo wa kusimamia utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi.
Amebainisha kuwa CCM imeendelea kutimiza malengo yake ya kuwaunganisha wananchi wote na kuwatumikia kwa weledi pasipo kuangalia itikadi zao za kisiasa, ikiwemo kujenga uhusiano mzuri na vyama rafiki vya nchi nyingine.
‘Tunajivunia kuwa na viongozi makini na wenye maono makubwa ya kimaendeleo, hii ndio CCM inayopendwa na watanzania, na itaendelea kuaminiwa, nashauri wenzetu wa upinzani waendelee kujifunza ili wajenge vyama vyao’, amesema.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa Mkoa huo Idd Moshi ametaja sababu kubwa ambayo inakifanya chama hicho kuendelea kukaa madarakani tangu kizaliwe ni kwa sababu kiko karibu zaidi na wananchi wake na kinajali sana maslahi yao.
Amesisitiza kuwa CCM itaendelea kuwa chaguo namba moja la wananchi, kutokana na mkakati wake wa kuhakikisha kero zao zinatatuliwa kwa wakati na kuhakikisha yale yote yaliyoelezwa katika ilani yake ya uchaguzi yanatekelezwa kwa vitendo.
More Stories
EWURA yatangaza bei kikomo za mafuta
Fainali Khimji cup kufanyika Februari 7,2025
Idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa hospitali Mnazi Mmoja yaongezeka