January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wamiliki wa Malori: Rais Samia amerahisisha mazingira ufanyaji biashara

Na Penina Malundo,TimesMajiraOnline,Dar

WAMILIKI wa Maroli Tanzania (TAMSTOA) wamesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameweka mazingira rafiki ya ufanyaji wa biashara nchini, hali inayochangia bandari ya Dar es Salaam kupokea meli nyingi.

Wamesema hali hiyo imeleta fursa kwao na kufanya kuwepo kwa idadi kubwa ya mizigo ambayo inahitajika kusafirishwa nje ya nchi.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa TAMSTOA, Chuki Shabani, wakati wa Mkutano Mkuu wa Nne wa mwaka wa wamiliki hao uliyowakutanisha wadau mbalimbali katika sekta ya usafirisha.

Amesema watu wasimkatishe tamaa Rais Samia kwa juhudi hizo anazozionesha. Alisema TAMSTOA kwa kushirikiana na Serikali inahitaji kuendelea kuhakikisha inaboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara nchini ili yaendelee kuwa bora zaidi.

Aidha, wanaiomba Serikali kutatua changamoto ya kukamatwa kwa maroli inayochangia kuchelewesha mizigo inayosafirishwa kwenda nje ya nchi.

Shabani amesema maroli yao yanabeba mizigo ya watu wa nchi za nje, hivyo ukamataji unaoendelea hasa katika Wilaya ya Temeke unakwamisha ufanyikaji wa biashara hiyo kwa wakati.

“Sisi maroli yetu yanabeba mizigo kupeleka nchi za nje, trafiki unapoyakamata na kukaa nayo zaidi ya saa tano kisa unamdai dereva faini ya sh. 50,000 ambayo kwa wakati hiyo anakuwa hana.

Ni bora kuachia gari iende kupeleka mzigo kisha irudi kuliko kuikamata kwa saa zaidi ya tano, ambazo angezitumia kufika hata Mbeya, tunaiomba Serikali kupitia jeshi la polisi kutusaidia kutatua changamoto hii kwa kuwapatia elimu watendaji,” amesema.

Ametaja changamoto nyingine kuwa ni usalama wa mizigo na madereva katika za Congo na Zambia limekuwa tishio katika utekelezaji wa biashara ya usafirishaji wa mizigo.

Rais Samia Suluhu Hassan

“Hali hii imesababisha matukio ya mara kwa mara ya utekaji wa magari ya mizigo inayosababisha hasara kwa wamiliki na madhara kwa madereva mfano kujeruhiwa na wengine kuuawa, ila tumeambiwa jambo hili linafanyiwa kazi,” amesema

Aidha amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia ni sikivu, kwani yapo mambo mengine ambayo yalikuwa yakiwakumba imeweza kuyatatua kwa wakati.

Akijibu changamoto ya kukamatwa kwa maroli, Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Barabara kutoka Wizara ya Uchukuzi, Andrew Magombana, amesema watakutana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ili kutatua jambo hilo kwa wakati.

“Tutakutana na wenzetu wa Tarura pamoja na Tanroads ili kuhakiksha changamoto hii ya kamatakamata ya maroli inatatuliwa kwa wakati, tuunaendelea na vikao nyetu vya kazi mapema tu tunalitatua jambo hilo na wenzetu waendelee na kazi kama kawaida,” alisema

Wamiliki wa malori

Aidha, amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia ipo pamoja na wamiliki wa maroli nchini hasa katika kuonesha nia dhabiti ya kusikiliza changamoto zao zinazowakabili na kuweza kuzitatua.

Kuhusu malipo kwa madereva, Magombana amesema kwa sasa kuna sheria rasmi kuhusu maslahi ya kundi hilo, hivyo amewataka madereva kwa umoja wao waifuate.