November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wamiliki wa ardhi kuanza kupokea ujumbe kupitia simu zao

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi imefanya maboresho katika mfumo mzima wa utunzaji kumbukumbu za ardhi, utozaji wa kodi na utoaji wa huduma za Sekta ya Ardhi ambapo wamiliki wa ardhi watapokea ujumbe kwenye simu zao za mkononi kuhusu huduma za ardhi na madeni yao.

Hayo yameleezwa jijini hapa leo,Aprili 21,2023 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi Dkt. Angelina Mabula wakati akizungumza wa Waandishi wa habari kuhusu maboresho mbalimbali yaliyofanyika kuhusu ulipaji wa kodi ya pango la ardhi na maduhuli mengine ya Sekta ya Ardhi.

Amesema lengo la maboresho hayo ni kurahisisha utoaji huduma, kuwapunguzia wananchi gharama za ufuatiliaji huduma na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali. 

“Maboresho hayo ni njia ya  kukabialiana na changamoto za wananchi kusafiri kwenda kwenye ofisi za Mikoa na Halmashauri ili kukadiria na kujua deni la msingi na riba itakayosamehewa kwani wengine walikuwa wanaona ni kupoteza muda na kupata usumbufu wakusubiri kupewa namba ya malipo(control number),”amesema Mabula.

Ametaja miongoni mwa maboresha yaliyofanyika  ni pamoja na kuboresha mifumo ili iweze kutuma ujumbe mfupi wa maandishi ambao hutumwa kwa wadaiwa wote kuwakumbusha kulipa kodi kwa wakati kupitia simu za viganjani. 

“Ujumbe unaotumwa kwa sasa umeainisha jina la mmiliki, taarifa za kiwanja, (namba ya kiwanja, kitalu na eneo kiwanja kilipo), namba ya utambulishoya mlipa kodi (lot ID), kiasi cha kodi  inayodaiwa, riba itayosamehewa, deni la msingi  na control namba ya kulipia deni husika,”amesema.

Waziri huyo  ameeleza kuwa Mkoa uliobaki ambao ni Dar es Salaam zoezi hilo linaendelea na ifikapo tarehe 30 Aprili, 2023 wamiliki wa ardhi katika Mikoa yote ya Tanzania Bara watakuwa wametumiwa jumbe kupitia simu za mkononi kuhusiana na madai ya kodi ya pango la ardhi.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inatarajia kuongeza mapato yanayotokana na sekta ya Ardhi ambapo matarajio ya zoezi hilo ni kuwa endelevu na litatekelezwa sambamba na kuendelea na maboresho ya mifumo. 

Mabula ameeleza kuwa hatua hiyo imekuja kutokana na  agizo la Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,  Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa msamaha wa riba ya malimbikizo ya pango la ardhi ambapo wananchi walio na malimbikizo wamepewa nafuu ya kulipa deni la msingi ili wasamehewe riba ya malimbikizo kuanzia Julai 2022 hadi Machi, mwaka huu.

Aidha Katika kipindi hicho, jumla ya wamiliki 9,188 walinufaika na msahaha huo ambapo shilingi bilioni 32 zilikusanywa ikiwa ni deni la msingi na shilingi bilioni 21.9 zilisamehewa ikiwa ni riba ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi.

Hata hivyo, Dkt. Mabula amesema baadhi ya wananchi walishindwa kunufaika na msamaha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo taratibu zinazowataka kufika katika ofisi za Ardhi ili kukadiria na  kujua deni la msingi  na riba itakayo samehewa. 

Amesema hadi sasa zaidi ya jumbe 84,000 za simu zimetumwa kwa wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi zikiwa na deni la msingi kiasi cha takribani bilioni 115 ambazo zinatarajiwa kukusanywa katika Mikoa 25. 

“Wananchi wakiona ujumbe katika simu ukianza na neno ARDHI wajue ni jumbe sahihi na zinatoka Wizara ya Ardhi zikiwakumbusha kulipa kodi kwa wakati ili wanufaike na msamaha uliotolewa na Mhe.Rais Dkt. Samia Suruhu Hassan na mwisho wa Msamaha ni tarehe 30 Aprili 2023,”amesema.