Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
MJUMBE wa Baraza la Wazazi Mkoa wa Mwanza, Alfred Wambura ‘Trump’,amechangia matofali 300 ya ujenzi wa ofisi ya Mtaa wa National Magharibi,katika mkutano wa kumpongeza Jumanne Mganga, Mwenyekiti wa Mtaa huo.
Wambura ametoa wito kwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliogombea uongozi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuachana na makundi na ili kuimarisha umoja na maendeleo ya chama hicho.
Amesisitiza kuwa uongozi ni suala la kupokezana kijiti,kwa kuwa uchaguzi umekwisha, ni muhimu kwa wanachama wa CCM kushirikiana kwa maslahi ya chama chao,kwani hakuna mwenye hati miliki ya nafasi yoyote ndani ya CCM, hivyo ni lazima waungane bila kujali makundi yao kabla ya uchaguzi.
“Haiwezekani ukawa mtu mmoja katika uchaguzi lazima muwe wengi hatimaye apatikane mshindi ili kazi iendelee,Trump alishindwa na Biden lakini ameshinda tena licha ya kufunguliwa kesi na kukoswakoswa risasi,leo ni Rais,”.
Amesema kuwa anatambua jinsi walivyofanya kazi ya kumshawishi Mganga kutoka CUF,kuja kujiunga na CCM akiwa mjumbe wa Serikali ya mtaa huo.
“Mimi,marehemu mzee Kafiti na Mpembenwe,tulifanya kazi kubwa ya kukutoa CUF,nafahamu ulipitia wakati mgumu hadi kupata nafasi hii,ni nadra kuchaguliwa kwa vipindi vitatu,”.
Kwa upande wake Jumanne Mganga,ambaye amechaguliwa kwa mara ya tatu kuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa National Magharibi,ametoa shukrani kwa wananchi na wanachama wa CCM, kwa kumuamini na kumpigia kura.
Ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa uaminifu,uadilifu na weledi wa hali ya juu huku akiwataka wananchi kumsaidia katika kuendeleza mtaa wao kwa kubuni miradi ya maendeleo.
Aidha,Mganga amesisitiza kuwa ushindi huo ni ishara nzuri kwani wapinzani walikubali kushindwa na kutosimamisha wagombea wao katika mtaa huo,waliona kuwa kuna uongozi bora na siasa safi chini ya CCM.
“Mwalimu Julius K. Nyerere aliwahi kusema maendeleo ya nchi yanahitaji watu,ardhi,siasa safi na uongozi bora.Wapinzani waliona kuwa CCM inaongoza kwa ufanisi na hivyo wakaamua kutosimamisha wagombea wao,”amesema.
Akisoma risala kwa niaba ya wananchi,Nicoline John amempongeza Mganga kwa kushinda tena kwa kishindo ambali amezungumzia changamoto za mtaa,ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ofisi ya mtaa,mahema (tents),viti na miundombinu mibovu ya barabara.
Hata hivyo,amesema wananchi wana haki ya kupokea maendeleo na si fedha,hivyo viongozi wa mtaa akiwemo mgeni rasmi wanapaswa kuzingatia hilo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Sheikh wa Wilaya ya Ilemela,Abdulwarith Juma,amewapongeza wagombea hao wa CCM,akisema kuwa wananchi baada ya kuwachgua kwa ridhaa yao wanahitaji maendeleo na si fedha,hivyo Mwenyezi Mungu awajalie nguvu ya kuyasimamia wanayotaka wananchi,na aliahidi kuchangia sh.50,000 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya mtaa.
Baadhi ya viongozi wa CCM Kata ya Nyakato wakiongozwa na Edward Malila na Masatu Mukabe ambaye ni mmoja wa wazee wa mtaa huo, pia wamesisitiza umuhimu wa kushirikiana kwa maslahi ya wananchi,kwa viongozi kutenda haki ili kuacha legacy (urithi) nzuri na kuendeleza ustawi wa mtaa wa National Magharibi.
Pia,katika mkutano huo wadau mbalimbali wameahidi kuchangia vifaa vya ujenzi wa ofisi ya mtaa yakiwemo matofali,saruji na mawe akiemo Joseph Ohondo aliyahidi matofali 100.
More Stories
Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu
RC Mrindoko:Ufyekaji wa mahindi Tanganyika si maelekezo ya serikali