November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waliougua ugonjwa wa kushindwa kupumua wanahitaji msaada wa kisaikolojia

Na Aveline Kitomary,TimesMajira Online,Dar es Salaam

MTAALAMU wa Saikolojia kutoka Taasisi ya AAR, Dk Bonaventure Balige amesema watu waliougua magonjwa ya tatizo la kupumua na nimoni wanahitaji msaada wa kisaikolojia ili kuweza kubadilisha mitazamo yao hasi kutokana na hali walizopitia.

Human Respiratory System Illustration. 3D render

Akizungumza na TimesMajira Online jijini Dar es Salaam, Dkt. Balige amesema watu wanaopitia nyakati ngumu hasa ugonjwa wanatakiwa kujua ukweli wa kile ambacho kiliwasumbua na kubadilisha mitazamo yao ili kurudi katika hali ya awali.

“Tatizo la kisaikolojia linaweza kumsumbua mtu kutokana na jinsi anavyolichukulia, kuna mwingine anaweza kuona kuwa atakufa hii inaweza kuwa na madhara katika saikolojia yake hata pale anapopona anakuwa na hisia mbaya.

“Hivyo ni muhimu watu kama hawa kupata ushauri wa kisaikolojia kwa kuelewa ukweli wa kile kilichowakuta na kusaidiwa kuondoa hofu iliyopo kwenye ubongo na akili zao,”amebainisha Dk Balige.

Amesema msongo wa mawazo husababishwa na matukio yanayotokea ambayo hufanya mpokeaji kuwa na mtazamo hasi au mbaya ambao husababisha hofu kubwa.

“Msongo wa mawazo (stress) ni maumivu yanayotokana na hisia ambazo zinatoka katika ubongo na akili, mtu akianza kufikiria kuwa korona itamuua ubongo utakuambia uko kwenye hatari kwani ubongo ndio unatengeneza hisia kama hofu,hasira,chuki na mengine.

“Baada ya kupokea taarifa fulani hisia zinachukua hatua hivyo ni muhimu watu kuepuka hofu kwani inaweza kuleta madhara katika mwili kama vile moyo,unaweza kupata magonjwa mengine kama kisukari,’stroke’ na mengine,”ameeleza Dkt.Balige.

Amesema kuwa njia nzuri ya kuondoa hofu ni kupata taarifa sahihi ambayo itamsaidia muhusika kuelewa kitu cha kufanya ikiwa ni pamoja na kujikinga.

“Katika vitabu imeandikwa kuwa ‘kweli itamweka mtu huru’ na mimi nasema ni vyema watu wakajua ukweli ili wawe huru hii itawasaidia katika saikolojia yao na kama kuna hofu lazima wasaidiwe wajue jinsi ya kujikinga.

“Napenda kuwaambia watu kuwa waepuke hofu kutokana na athari zake hata wale waliopoteza ndugu wapate ushauri wa kuondokana na hofu,”ameshauri Dt. Balige.