Na Rotary Haule,TimesMajira online,Kibaha
WAFUNGWA wawili waliosamehewa kifungo chao Aprili 12, mwaka huu na Rais Samia Suluhu Hassan, wameuawa kwa kushambuliwa na wananchi wakituhumiwa kuiba vitu mbalimbali.
Wafungwa hao kabla ya kusamehewa walikuwa wakitumikia adhabu yao katika Gereza Mkuza lililopo Kibaha, mkoani Pwani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa,amewaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake kuwa tukio mauaji ya watu hao yalitokea Mei 8, mwaka saa 12 alfajili maeneo ya Kibaha kwa Mathias .
Nyigesa, amewataja watu hao kuwa Ramadhani Mohamed (28) mkazi wa kwa Mathias Kibaga na Idd Hamis (30) mkazi wa Jamaika Kibaha.
Amesema siku chache baada ya wafungwa hao kusamehewa na Rais na kurudu uraiani, waliendeleza tabia ya wizi katika katika maduka na maeneo mbalimbali, lakini waliingia mikononi mwa wananchi na hivyo kupata kipigo.
Alisema kuwa,watu hao baada ya kukamatwa na wananchi hao walipigwa kwa kutumia silaha za jadi, mawe, mapanga na fimbo, ambapo waliumia vibaya na kwamba walifariki wakiwa njiani wakati wakiwa wanapelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Kamanda Nyigesa ametoa rai kwa wananchi kuacha kuchukua sheria mkononi na badala yake wawaachie vyombo vya dola kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria .
Katika hatua nyingine Jeshi hilo limefanya operesheni katika kipindi cha wiki moja katika wilaya tano za Kipolisi na kufanikiwa kukamata watuhumiwa 21 wakiwemo wanawake watatu.
Kamanda Nyigesa,amesema watu hao wamekamatwa wakiwa na vitu mbalimbali vya wizi walivyoiba katika maeneo tofauti ya Mkoa wa Pwani.
Nyigesa,alitaja baadhi ya vitu vilivyokamatwa kuwa ni televisheni nne simu za mkononi tatu, kompyuta mpakato mbili aina ya Aple na Dell,Radio aina Kenwood, pikipiki , ng’ombe wawili,na vifaa vingine vya umeme.
Hata hivyo, Nyigesa amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wananchi katika kufichua taarifa mbalimbali za waharifu.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
HAYA HAPA MATOKEO YOTE FORM II NA DARASA LA IV
Ufaulu waongezeka matokeo ya Darasa la Nne na Kidato cha Pili