December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waliopoteza mikono kuwekewa mikono bandia bure

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda Mbeya imewaomba wananchi waliopoteza mikono kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ajali kuendelea kujitokeza katika hospitali hiyo ili kuwekewa mikono bandia inayotolewa bila malipo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali Rufaa Kanda ya Mbeya,Dkt.Godlove Mbwanji amesema kuwa kambi itadumu kwa siku nne katika hospitali hiyo ambapo huduma itatolewa na hospitali kwa kushirikiana na wadau kutoka nchi za Ghana ,Sudan na Uganda.

“Zoezi hili la uwekaji mikono bandia limeanza Desemba 8 mwaka huu na tunategemea litadumu kwa siku nne hospitali hapa ,hivyo tunaomba wananchi waliopoteza mikono yao kutoka maeneo yote ya mikoa ya mbali wafike wapate huduma,hapa zoezi hili tumeanza leo lakini tumepokea watu waliopoteza mikono yao kutoka mikoa mingine na wamepatiwa huduma hii “amesema Dkt.Mbwanji.

Aidha Dkt.Mbwanji amesema hiyo imeanza kutoa huduma ya kuwasaidia watu waliopoteza mikono kwa ajali au changamoto nyingine kwa kuwapatia mikono bandia,kuwasaidia kuifunga kabisa ili iwawezeshe kufanya shughuli zao kama ilivyokuwa awali ambapo zoezi hili linafanywa kwa kushirikiana na huduma ya the hell project ambayo yenyewe inatolewa nchini Ujerumani ambako ndipo makao makuu,”amesema.

Pia matarajio ni kwamba zoezi hilo linapofanyika watatoa mafunzo kwa watalaam wazawa ili kuwawezesha kufanya huduma hii iwe endelevu baada ya siku hizi nne za zoezi maana yake wataendelea kuratibu kwa kuchukua majina ya watu wenye uhitaji wa mikono bandia .

Hata hivyo Dkt.Mbwanji amesema kuwa wataalamu hao wamejitolea kusaidia hospitali ya rufaa ya Kanda kuleta mikono bandia na vifaa vyake bila malipo hivyo wataendelea kutoa huduma hata baada ya siku nne kuisha hivyo ni vema wale watu wenye ulemavu au waliopoteza viungo kwa ajali wafike hospitali kupata huduma hiyo.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa Dkt.Lunemo Sakafu amesema kuwa wamelenga kufikia watu wote ambao watapata taarifa kwani walitoa namba za simu ambazo wanawasiliana nao kuwapa taratibu za kufika hospitali.

Dkt.Sakafu amesema kuwa mikono hiyo bandia watakayowawekea watafundishwa kuvaa na kubadilisha pindi wanapotaka kuvaa au kufanya shughuli yeyote.

Akielezea mwitikio wa watu kujitokeza amesema wameweka mikono watu kutoka Iringa,Dar es Salaam,Singida na Mwanza na kushukuru vyombo vya habari kwa kusambaza taarifa.

“Wananchi wengi tuliowapokea hapa kuja kuweka mikono bandia asilimia 75 wamekatika mikono kutokana na ajali za gari,bodaboda na wachache wenye ulemavu wa kuzaliwa”amesema

Juma Abdallah mkazi Kibaha Ruvu Juu amesema kuwa chanzo cha kukatika mkono huo ni baada ya kukamatwa na mamba akiwa anavua samaki mwaka 1993 ,hivyo ameshukuru kupata mkono wa bandia ambao utakuwa msaada mkubwa katika shughuli zake za kila siku za uzalishaji mali na za kujiongezea kipato.