Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Dar
JUMLA ya wanawake na wasichana 27 wamefanyiwa upasuaji wa kurejesha uwezo wa kutembea na kukunjua viungo, vilivyokakamaa ambao walipata ulemavu kutokana na majeraha ya moto, ukatili wa kijinsia na ajali.
Novemba 29 hadi Desemba 6 mwaka huu hospitali ya Aga Khan kwa kushirikiana na Reconstructing Women International (RWI) na hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),wamefanya upasuaji wa plastiki wa kurekebisha maumbile katika awamu ya tisa ya programu hiyo endelevu iliyoanzishwa mwaka 2016.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Daktari Bingwa wa upasuaji na Mkuu wa Idara ya upasuaji katika hospitali ya Aga Khan, Dk. Athari Ali,amesema mpango huo unalenga kurejesha uwezo wa kimwili ili kuleta nguvu na kuboresha ubora wa maisha ya wanawake na wasichana nchini.
Amesema katika awamu tisa zilizopita kati ya mwaka 2016 hadi mwaka 2023 zaidi ya wagonjwa 300 walinufaika na upasuaji huo wa bure,pia madaktari 16 wa upasuaji wa kurekebisha maumbile, upasuaji wa jumla na wanafunzi wa tiba kutoka hospitali mbalimbali za umma na binafsi wamepata mafunzo kupitia mpango huo.
“Wengi wa madaktari hawa wa ndani sasa wanaweza kutoa upasuaji wa kurekebisha mwili katika hospitali za umma. Kutokana na wingi wa wagonjwa hawa nchini,taasisi ya huduma za afya ya Aga Khan na washirika wake wanakusudia kupanua kambi za mpango huu kutoka mara moja kwa mwaka hadi mara mbili kwa mwaka,”amesema Dkt.Ali.
Naye Daktari Bingwa wa upasuaji wa kurekebisha mwili kutoka MNH, Edwin Mrema,amesema kadri idadi ya watu nchini inavyoongezeka mahitaji ya huduma maalum za afya ikiwa ni pamoja na upasuaji wa kurekebisha mwili yanazidi kuongezeka.
Amesema ili kukabiliana na suala hilo serikali inashirikiana na hospitali ya MNH na mashirika ya kimataifa ikiwemo RWI.
Ushirikiano huo unalenga kujenga uwezo wa madaktari wa ndani, kuboresha upatikanaji wa vifaa vya kisasa na kuleta madaktari wataalamu kutoka nje ya nchi.
Daktari Bingwa wa upasuaji wa kurekebisha mwili ambaye ni kiongozi wa timu ya RWI, Andrea Pusic,amesema wamekuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa wanawake na wasichana wengi waliokumbwa na majeraha ili kuboresha uwezo wao wa kimwili na muonekano mzuri.
Naye Daktari Bingwa wa upasuaji kwa matundu madogo katika hospitali ya Aga Khan, Aidan Njau,amesema wagonjwa hao huwapata mikoani na kuangalia walioumia kwa kiwango kikubwa ili kuwapatia huduma hiyo ya upasuaji na kuwarejeshea tumaini na tabasamu kwa wanawake na wasichana wa Tanzania.
“Yupo mwanamke ambaye titi lake lilisagika huyu tulimfanyia upasuaji na kwa sasa mgonjwa yupo katika hali nzuri,alikosa matumaini ya kupona na wengine waliopata majeraha makubwa kutokana na ajali za gari hali iliyowasababishia kupata ulemavu wamepona,”amesema Dk. Njau.
Amesema programu hiyo hufanyika kila mwaka na madaktari maalum kutoka Ulaya na Marekani hutoa huduma na mwitikio kwa wananchi ni mkubwa.
Dkt Njau,amesema matibabu yanayotolewa huwa ni gharama kubwa lakini wanayatoa bure kwa wananchi, hivyo Watanzania wachangamkie fursa hiyo ya matibabu.
More Stories
Wizara ya Nishati yawasilisha utekelezaji wa bajeti 2024/2025 kwa Kamati ya kudumu ya bunge Nishati na Madini
Watanzania milioni 13.5 kusambaziwa umeme ifikapo 2030 kutoka milioni 5.2 ya sasa
Mhandisi Kundo agoma kuweka jiwe la msingi mradi wa maji