March 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walimu waaswa kutowatenga watoto wenye ulemavu

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

WALIMU wa Elimu Maalum mkoani Mbeya wameaswa kutowatenga watoto wenye ulemavu katika shule zinazofundisha watoto hao na badala yake wawapokee kwa mikono miwili kama walivyo wengine katika kutekeleza mpango wa elimu Jumuishi.

Hayo yamesemwa Machi 5,2025  na Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Mbeya,Maftaha Vedastus wakati wa kikao maalum kuhusu elimu jumuishi kilichoitishwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Child support Tanzania na kuwakutanisha maafisa elimu  kata na Msingi,walimu,madiwani pamoja na
waandishi habari

Vedastus amesema kuwa Mkoa wa Mbeya una jumla ya shule 1,056 na kati hizo msingi 856, na Sekondari 287 Shule zote zinapokea watoto wote wenye ulemavu ila inategemeana na kiwango cha mahitaji hivyo wanapokuja katika Shule zenu muwapokee kwa mikono miwili na msiwatenge.

“Watoto hawa wanapokuja kwenye shule zenu jitahidini kuwapokea vizuri na msiwatenge lakini ndugu zangu waheshimiwa Madiwani mnapokaa kwenye vikao vyenu vya bajeti semeni na mrejee je mmewahi kutembelea hata shule moja ya mahitaji maalum tutembelee Mwenge pale tukaone watoto wetu.

“Mkoa unataka kujenga shule ya mahitaji maalum kuanzia msingi mpaka Sekondari wakati inajengwa na sisi huku tuwe na vitu  vya kuzungumza kuhusu watoto wetu katika suala la elimu jumuishi”amesema

Akizungumzia kuhusu suala la watoto wenye ulemavu,Kaimu Ofisa Elimu huyo amewataka walimu wanaofundisha watoto hao  kuwatembelea majumbani watoto wenye mahitaji hafifu ili kuwafundisha namna ya kujihudumia pamoja na kufahamu changamoto zingine zinazowakabili.

“Ni wangapi wamewatembelea watoto hawa na kufika kwa wakuu wa Shule kuomba ruhusa kuwatembelea watoto hawa kuona maendeleo yao,tufike tuone unaweza kuta watoto hawa wapo stoo wamefungiwa inaumiza kwa hiyo tukipata wadau kama child support Tanzania tuwatumie ipasavyo na sisi kama mkoa tutapita kusisitiza na kufuatilia utekelezaji kwa fani yetu ya elimu maalum kila leo mambo yanabadilika basi tuingie hata kwenye mitandaoni kwenye zile programu zetu za mafunzo ya walimu kazini tutakuta vyote hivyo”amesema.

Doreen Mayani ni Mratibu Miradi Child support Tanzania amesema kuwa mradi huo unatekelezwa chini ya Shirika la Haki Elimu na mradi huo umejikita kwenye mikoa minne na kutekelezwa na mashirika matano ikiwemo Dar es Salaam kwa shirika linaitwa kooden , Mbeya, child support Tanzania,Morogoro mashirika mawili ,na
Mtwara hivyo mashirika matano yamepewa majukumu ya utekelezaji mzima mkakati wa mpango wa elimu jumuishi.

Mayani amesema kwamba mpango mkakati huo unatekelezwa kwa awamu ya pili ambapo mara ya kwanza ulitolewa ukaonekana kuwa na mapungufu na haukutekelezwa kwa ufanisi na hivyo ukatolewa mpango mkakati mwingine wa awamu ya pili ambao unatekelezwa na unatarajia kuisha mwaka 2026 na je umetimiza malengo ambayo serikali na wadau walikaa na kutathimini wakaona ili kuwasaidia watoto wote wenye mazingira tofauti tofauti.

Mwalimu wa shule ya Msingi Mwenge,Aness Mwakaje amesema kuwa jamii bado haikubali kuona watoto wao walivyo hivyo tuombe jamii ielimishe wazazi kukubaliana kuwa watoto walivyo ni dhambi bali ni jinsi Mungu alivyopanga wakubali kusaidiwa mpaka inafika wakati inabidi watoto wapandishwe madarasa ambayo hawastihili wakati uwezo wao ni kuishia darasa la nne tu hivyo elimu inatakiwa kuzidi kutolewa na luwapa matumizi wazazi kuona kuwa ni hali ya kawaida kuwa watoto hao ni kama walivyo watoto wengine.