Na Adili Mhina
Walimu wametakiwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na kuzingatia miiko na maadili ya kazi hiyo ili kufikia malengo ya Serikali katika kuogeza ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama katika ziara yake wilayani Iramba ambapo alifanya mkutano uliowahusisha Walimu, Wakuu wa Shule, Mwakilishi wa CWT, Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC Iramba, Waratibu Elimu Kata, Wathibiti Ubora, Mwenyekiti wa Kamati ya TSC Wilaya ya Iramba pamoja na Maafisa Elimu wa Msingi na Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kutoa elimu kwa wadau wa sekta ya elimu juu ya masuala mbalimbali ya sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa walimu ili kuongeza kasi ya utendaji kazi wa walimu.
Nkwama alieleza kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi katika sekta ya elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora, hivyo walimu hawanabudi kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu ili kupata matokeo yanayoendana na thamani ya fedha inayowekezwa.
“Lengo letu Kitaifa kwa upande wa taaluma ni kuhakikisha asilimia 90 ya wanafunzi wanaohitimu darasa la saba wanafaulu. Kwa kuwa Iramba ni miongoni mwa Halmashauri zilizopo vijijini, lengo lenu ni kuhakikisha asilimia 85 ya wanafunzi wanafaulu ikiwa ni pamoja na kumudu stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (kkk),” amesema.
Kwa upande wa sekondari, Nkwama alieleza kuwa ipo changamoto ya upungufu wa walimu katika masomo ya sayansi na hisabati lakini walimu wa masomo ya sanaa wapo kwa kiwango kikubwa, hivyo endapo walimu hao watatekeleza wajibu wao vizuri, hakuna mwanafunzi atakayepata chini ya daraja la tatu kwenye matokeo ya mitihani ya Taifa.
“Walimu wa Kiswahili, English, History, Geography na Civics tupo, hivyo tunatarajia kiwango cha chini cha ufaulu kwa kila somo kwa mwanafunzi kiwe ni C. Mwanafunzi akiwa na C tano tayari ana division three hapo tutakuwa tumeondokanana division four na zero,” amesema.
Pamoja na malengo hayo ya ufaulu, Nkwama alisisitiza kuwa wanafunzi wanatakiwa wafaulu kwa haki na sio kutumia mbinu za udanganyifu wa mitihani jambo ambalo sio kwamba tu ni kinyume na sheria na taratibu za kazi bali pia linabomoa Taifa.
Alieleza kuwa walimu ndio wenye jukumu kubwa la kufanya malengo hayo yafikiwe, hivyo suala la nidhamu na maadili ni la msingi kwa kuwa mwalimu asiye na maadili hawezi kutimiza wajibu wake kama alivyopangiwa na serikali.
“Mwalimu anayezingatia maadili ya kazi yake ndiye anayeweza kufanya kazi kwa bidii na kujituma. Mwalimu asiye na maadili atakuwa mvivu, mzembe na asiyejali kazi yake. Hivyo maadili na nidhamu ni jambo la kwanza katika kufikia malengo yaliyokusudiwa,” alisisitiza.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake katika Mkutano huo, Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC wilayani hapo, Francis Kasian alieleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ina jumla ya walimu 1,139 wa shule za msingi na sekondari wanaofundisha shule za serikali.
Alisema kuwa kuanzia mwaka 2016 ofisi yake imeshughulikia mashauri ya nidhamu 61 ambapo mashauri 41 yalikuwa ni ya makosa ya utoro, 16 mahusiano ya mapenzi na wanafunzi na mashauri 4 yalikuwa ya makosa mbalimbali ya ukiukaji wa maadili ya kazi ya ualimu.
“Katika kushughulikia mashauri hayo, walimu 33 walifukuzwa kazi na 28 walipewa adhabu mbalimbali zikiwemo kupunguziwa mshahara, kushushwa cheo na kusimamishiwa nyongeza ya mshahara baada ya kukutwa na hatia,” alifafanua.
Kasian alihitimisha kwa kusema kuwa kumekuwa na ushirikiano wa karibu kati TSC na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo katika kuwafikia walimu na kuwaelimisha juu ya masuala mbalimbali ya utumishi wao, jambo ambalo limefanya mashauri ya nidhamu kuendelea kupungua.
Kwa pande wake Mwenyekiti wa Kamati ya TSC Wilaya ya Iramba, Shiwariael Marunda alieleza kuwa Kamati yake imekuwa ikifanya jitihada za maksudi katika kuwaelimisha walimu ili wasijiingize katika makosa ya kiutumishi.
“Tukiwa kwenye vikao vya kamati yetu, hakuna kitu kinachotuumiza kama kupokea shauri la nidhamu ambalo ukiliangalia linakwenda kupoteza ajira ya mwalimu. Kwa kweli tumejikita sana katika kuwaelimisha walimu waelewe sheria na taratibu za utumishi wao,” amesema.
Naye Katibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Manasseh Stephen alieleza kuwa kuna baadhi ya walimu ambao walipata barua za kupandishwa vyeo mwaka 2016 lakini barua hizo zikafutwa kutokana na zoezi la uhakiki wa watumishi hewa na kuomba serikali iwasaidie walimu hao waweze kupanda vyeo katika zoezi linaloendelea sasa.
“Ndugu Katibu kwa kuwa walimu hawa walichelewa kupanda madaraja katika kipindi cha nyuma baada ya kufutiwa barua walizokuwa wamepewa awali, ninaomba muishauri Serikali ili walimu hao waweze kupanda vyeo katika zoezi la sasa,” alisema Stephen.
Katika mkutano huo mada mbili ziliwasilishwa ambapo Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC Makao Makuu, Christina Hape aliwahimiza walimu kuzingatia Nguzo za kazi ya ualimu ambazo zinamtaka mwalimu malezi na taaluma bora kwa wanafunzi, kuwajibika kwa mwajiri wake, kuwajibika kwa Taifa pamoja na kuwa na uzalendo.
Katika mada nyingine iliyowasilishwa na Afisa Utumishi anayeshughulikia masuala ya Ajira na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC Makao Makuu, Francis Gwankisa alieleza kuwa mwalimu anayekaribia kustaafu anatakiwa kuomba kibali cha kustaafu miezi sita kabla ya tarehe yake ya kustaafu ili kuondoa usumbufu kwa mfuko wa hifadhi ya jamii katika kushughulikia mafao yake.
More Stories
Tanzania,Uturuki kushirikiana kuinua sekta ya utalii nchini
Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu