November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walimu nchini kunufaika na mikopo ya NMB

Na Yusuph Mussa, Korogwe

MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Basila Mwanukuzi ameipongeza BenkiI ya NMB kwa mpango wake wa kuwakopesha mikopp yenye riba nafuu walimu kwa ajili ya kujiendeleza kielimu wao na watoto wao, kufanya biashara ndogondogo, ujenzi, vyombo vya moto kama bodaboda na bajaj.

Lakini pia kupata mkopo wa Bima yaani Insurance Premium Finance (IPF), ambayo inawezesha walimu kulipa bima kujikinga na majanga mbalimbali, mikopo ya pembejeo na mashine za kilimo, fursa za kushiriki promosheni na kujishindia zawadi mbalimbali na elimu ya kifedha kwa walimu.

Aliyasema hayo Julai 12, 2022 wakati anafungua Kongamano la Walimu na Benki ya NMB lililofanyika mjini Korogwe, na kuwashirikisha walimu na maofisa elimu 150 kutoka halmashauri zote 11 za Mkoa wa Tanga.

“Napongeza Benki ya NMB kutoa mikopo kwa ajili ya kuwaendeleza walimu. Mikopo hiyo itawasaidia walimu kujiendeleza wao na watoto wao, lakini pia kupewa mikopo ya kufanya biashara. Benki ya NMB, pamoja na kwamba ni benki ya biashara, lakini bado inatoa huduma za kijamii. Na kwa kuwasaidia walimu hawa ambao ni kundi kubwa, na sisi wote tumefundishwa na wao, mikopo hiyo itawasaidia kuboresha maisha yao wakiwa kazini na baada ya kustaafu” alisema Mwanukuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi huo, Mwanukuzi alisema mikopo hiyo itakayotolewa na NMB itaondoa kero za walimu kukopa mikopo umiza kutoka kwa baadhi ya taasisi, hivyo mikopo hiyo italeta utulivu kwa walimu na kufanya kazi zao kwa kujiamini, huku wakijiingizia kipato” alisema Mwanukuzi.

Meneja Mwandamizi Kitengo cha Wateja Binafsi Makao Makuu ya Benki ya NMB, Ally Ngingite alisema tafiti zinaonesha kati ya Watanzania milioni 60, ni asilimia 40 tu ndiyo wenye akaunti za benki. Lakini pia zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanamiliki simu za mkojoni, na wana uwezo wa kufanya malipo na miamala kupitia simu zao za mkononi.

“Kwa kutambua hilo, Benki ya NMB imeendelea kuja na masuluhisho mbalimbali yanayohusu makundi tofauti tofauti kama hili la walimu kama njia mojawapo yakuleta Watanzania zaidi kwenye mifumo rasmi ya kifedha na kupatia Serikali mapato. Kupitia masuluhisho haya, benki imeweza kufikisha asilimia 94 ya miamala yake kupitia simu za mkononi.

“Hivi karibuni tumezindua huduma kubwa tatu ambazo zinaendelea kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya kibenki Tanzania. Huduma hizi ni mikopo ya kidijitali (Mshiko Fasta), NMB Pesa Wakala na NMB Lipa Mkononi. Kupitia mifumo hii, tunaweza kuwafikia Watanzania wengi zaidi, na hivyo kuchangia kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za kibenki, na pia hata kuwasaidia walimu ambao wanaweza wakawa mbali na matawi ya benki” alisema Ngingite.

Ngingite alisema ndiyo maana Benki ya NMB wanasema: “Mwalimu Spesho- Umetufunza Tunakutunza”. Hivyo anawakaribisha walimu wote nchini kuchangamkia fursa hiyo.

Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kijungumoto Edward Katisho alisema Benki ya NMB ni msaada mkubwa kwao, kwani pamoja na mambo mengine, imewahi kuwachangia bati 180 na mbao 38 vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni tano kwa ajili ya kupaua vyumba vitatu vya madarasa.

Katisho alisema, hata mpango huo wa Benki ya NMB waliokuja nao sasa, utawasaidia walimu kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi, kwani pamoja na mikopo ya elimu, biashara ikiwemo kukopeshwa bajaj na pikipiki, bado kuna huduma za malipo kama umeme na maji, ambapo kupitia Benki ya NMB hakuna makato.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Mazoezi- Mbeza Aloycia Kessy alisema kongamano hilo limewapa mwanga wa kufanya biashara vizuri. Kumbe ukiwa mjasiriamali unapata fursa nyingi kuliko mfanyabiashara, hivyo kwa kiasi kikubwa, Benki ya NMB itainua maisha ya walimu na familia zao kwa kiasi kikubwa.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Basila Mwanukuzi (kushoto) akifungua Kongamano la Walimu na Benki ya NMB iliyofanyika mjini Korogwe na kuwashirikisha walimu, maofisa elimu ngazi ya kata na halmashauri takribani 150. Wengine ni Ally Ngingite, Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya NMB Makao Makuu (kulia), na Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kaskazini Dismas Prosper (katikati). (Picha na Yusuph Mussa).
Kongamano la Walimu na Benki ya NMB lililofanyika mjini Korogwe na kuwashirikisha walimu, maofisa elimu ngazi ya kata na halmashauri takribani 150. (Picha na Yusuph Mussa)
Kongamano la Walimu na Benki ya NMB lililofanyika mjini Korogwe na kuwashirikisha walimu, maofisa elimu ngazi ya kata na halmashauri takribani 150. (Picha na Yusuph Mussa)